Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Jude Bellingham amemsifia mshambuliaji mwenzake, Vinícius Júnior akisema kwamba yeye na Vinicius ni ‘pacha’ bora duniani.
“Kwangu huenda ndiye bora duniani, ni mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji vya juu niliyewahi kucheza naye,” alisema Bellingham alipoulizwa kuhusu Vinicius Jr.
“Mimi mwenyewe najiamini lakini sikujua kama ningekuwa katika ubora namna hii, nawapongeza wachezaji wenzangu na maofisa katika klabu,” alisema Bellingham.
Bellingham na Vinicius Jr wamekuwa wakicheza pamoja katika mechi za hivi karibuni baada ya Vinicius Jr kukosa mechi kadhaa kwa kipindi cha mwezi mmoja kutokana na matatizo ya misuli.
Kwa upande wake kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alisema kwamba walimwambia Vinicius aangalie eneo analoona akicheza atakuwa vizuri na kilichotokea ni kwamba yeye na Bellingham umekuwa muunganiko bora.
“Nafikiri wana muunganiko bora, wana ubunifu mwingi, tunapokuwa nao pamoja upande wa kushoto wanakuwa hatari,” alisema Ancelotti.
Ancelotti pia alimsifia Bellingham akisema kinachomshangaza yeye na bila shaka watu wengine kwa mchezaji huyo ni umri wake wa miaka 20 lakini mambo anayofanya ni kama vile ana miaka 30.
Katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Napoli hivi karibuni, Real Madrid ilitoka na ushindi wa mabao 3-2 na Vinicius Jr na Bellingham walicheza katika kiwango cha juu na kila mmoja alifunga bao katika mechi hiyo ambapo bao la Vinicius lilitokana na pasi ya Bellingham.