Montpellier, Ufaransa
Mechi ya Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1 kati ya Montpellier na Clermont iliyokuwa ikichezwa leo Jumapili imelazimika kusitishwa baada ya baruti kurushwa na kutoa moto uliolipuka karibu na kipa wa Clemornt, Mory Diaw.
Tukio hilo lilitokea katika dakika za majeruhi wakati wenyeji wa mchezo huo, Montpellier wakiwa mbele kwa mabao 4-2 na baada ya moto huo kurushwa na kulipuka kipa huyo aliyekuwa akijiandaa kupiga mpira alianguka.
Baada ya tukio hilo kipa huyo alipatiwa matibabu uwanjani lakini muda mfupi baadaye alibebwa kwenye machela na kutolewa nje na hapo hapo mechi ikamalizwa baada ya waamuzi kufanya kikao kidogo.
“Madaktari waliompatia matibabu kipa wa Clermont walithibitisha kwamba hakuwa katika hali ambayo ingefaa kwake kurudi uwanjani na kwa mantiki hiyo mechi imesitishwa,” alisema mmoja wa waamuzi wa mechi hiyo.
Montpellier huo ulikuwa ushindi wa kwanza wa nyumbani msimu huu hadi tukio hilo linatokea licha ya kucheza na wachezaji 10 uwanjani baada ya mchezaji wao, Maxime Esteve kupewa kadi nyekundu.