Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic amewashangaa wanasoka wanaokwenda Saudi Arabia kucheza soka kwa kuwa wanajiweka katika mazingira ya kufuta historia yao kwa kutojali vipaji vyao na kuangalia pesa.
Ibrahimovic (pichani) aliyewahi kuzichezea klabu za AC Milan, Man United, PSG na nyinginezo na kutwaa tuzo mbalimbali zikiwamo za ufungaji, alisema aliwahi kupata ofa za kucheza China na Saudi Arabia lakini hakuzipa nafasi.
“Nafikiri wachezaji waliofikia kiwango fulani wanatakiwa kuachana na soka wakiwa katika kiwango fulani cha juu,” alisema brahimovic ambaye alistaafu soka Juni mwaka huu akiwa anaichezea AC Milan.
Wachezaji kadhaa maarufu wakiongozwa na Cristiano Ronaldo, Riyad Mahrez, Karim Benzema, Jordan Henderson na wengineo wametimkia Saudi Arabia katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Klabu za Ligi Kuu Saudi Arabia au Saudi Pro Ligi, zimekuwa mstari wa mbele kwa kusajili wanasoka mastaa wa Ulaya kwa bei mbaya na klabu zilizo mstari wa mbele zikichuana katika mpango huo ni nne za Al Nassr, Al-Ahli, Al-Hilal na Al-Ittihad.
“Nilikuwa na ofa ya kwenda China, pia nilikuwa na ofa ya Saudi Arabia lakini hapo ni suala la nini unachotaka? Una malengo gani? Unatakiwa ukumbukwe kwa kipaji chako na si pesa ulizovuna,” alisema Ibrahimovic.
“Tunafanya mazoezi ya kila siku ya nini, kinachotufanya tutambulike ni vipaji vyetu na hicho ndicho unachotakiwa kukumbukwa nacho,” alisema Ibrahimovic.
“Huwezi kwenda kwenye ligi ya chini kumalizia maisha yako ya soka kwa namna tofauti, lakini kuna wachezaji wanahitaji mazingira ambayo yatawafanya waingize pesa nyingi kwa sababu hawakupata za kutosha,” alisema.
Katika hatua nyingine Ibrahimovic alisema kwamba hana tatizo na mambo mengine ya nje ya soka ambayo Saudi Arabia inalalamikiwa ikiwamo kinachodaiwa kuwa ni ukandamizaji wa haki za binadamu na kupinga mapenzi ya jinsia moja.
“Sikiliza, popote unapokwenda kucheza soka, ni soka, soka linaunganisha watu, ni ndoto ya pamoja, ukiwa mchezaji profesheno wa soka, kinachokuhusu ni soka, unapocheza soka hiyo inatosha, Na Saudi wamekuwa katika hilo,” alisema Ibrahimovic.
“Lakini mambo ya maadili? Hapana hayo tunafanya sisi wenyewe na familia zetu, nani atakuzungumzia miaka mitano au 10 unapokuwa na mali, na mwenye afya?” alihoji Ibrahimovic.