Na mwandishi wetu
Ihefu FC imeendelea kuwa mfupa mgumu mbele ya Yanga baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Highland Estate leo Jumatano.
Hii ni mara ya pili Ihefu inaendelea kuwa kikwazo kwa Yanga, msimu uliopita kwenye mechi ya ligi hiyo hiyo, Ihefu pia ilifanikiwa kuichapa Yanga mabao 2-1.
Matokeo hayo ya msimu uliopita yaliyowanyong’onyeza zaidi mashabiki wa Yanga kwa kwa timu yao ilikuwa ikisaka rekodi ya kucheza mechi 50 bila kupoteza hata moja lakini ikakwama mbele ya Ihefu na hivyo kubaki na rekodi ya mechi 49 bila kupoteza hata moja.
Msimu huu pia Yanga imeuanza kwa rekodi nzuri ya ushindi wa mechi tatu za ligi kwa kutoa vipigo vikali huku ikishika usukani wa ligi lakini Ihefu leo imekuwa kikwazo kwa kuinyima pointi hata moja.
Matokeo hayo yanaweza kuwa mwanzo wa timu hiyo kushushwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na mahasimu wao, Simba ambao kesho Alhamisi wataumana na Prisons mjini Mbeya.
Katika mechi ya leo Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao mapema dakika ya nne tu ya mchezo mfungaji akiwa ni Pacome Zouazoua, bao ambalo liliamsha shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo walioamini kazi ilikuwa imeanza dhidi ya Ihefu.
Zikiwa zimebakia dakika tano kabla ya timu kwenda mapumziko, Ihefu walisawazisha bao hilo kupitia kwa Lenny Kisu na kuzifanya timu ziende mapumziko zikiwa sare.
Katika dakika ya 65, Charles Ilanfya alizima ndoto za Yanga baada ya kuifungia Ihefu bao la pili na la ushindi lilitosha kuwatoa uwanjani mashabiki wa Yanga wakiwa vichwa chini.
Ushindi huo unaifanya Ihefu kufikisha pointi sita katika ligi hiyo wakati Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wanabaki na pointi zao tisa.
Soka Ihefu mfupa mgumu kwa Yanga
Ihefu mfupa mgumu kwa Yanga
Read also