Na mwandishi wetu
Licha ya mshambuliaji mahiri wa Simba, Jean Baleke kutoka akiwa na majeraha kwenye mechi ya mwisho ya timu hiyo, imeelezwa kuwa anaendelea vizuri na tayari amerejea mazoezini kwa mechi zijazo.
Baleke alishindwa kuendelea na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika juzi Jumapili dhidi ya Power Dynamos baada ya kuumizwa kwenye kifundo cha mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Willy Onana.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam iliisha kwa sare ya bao 1-1 na Simba kutinga hatua ya makundi kutokana na faida ya mabao ya ugenini ya mechi ya awali iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Akizungumza na GreenSports leo Jumanne, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema mchezaji huyo raia wa DR Congo anaendelea vizuri na leo ameanza mazoezi kwa ajili ya mechi mbili za Ligi Kuu NBC zinazofuata dhidi ya timu za Prisons na Singida Fountain Gate.
“Baleke yuko salama, alishaangaliwa kulingana na jeraha alilokuwa amelipata na yuko vizuri, leo (jana) tayari ameanza mazoezi na wenzake kwa ajili ya mechi zinazokuja, japokuwa ilionekana ameumia pakubwa lakini alipata maumivu madogo tu,” alisema Ally.
Mbali na Baleke, Ally alisema majeruhi wengine kama kipa Aishi Manula na Aubin Kramo nao wanaendelea vizuri ingawa hawajafahamu lini watarejea moja kwa moja kwenye majukumu ya kikosi hicho.