Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amemtaka mshambuliaji wake anayeandamwa na ukame wa mabao, Marcus Rashford kufanya bidii na kuwa makini kama anataka kuanza kuzifumania nyavu.
Msimu uliopita ulikuwa mzuri kwa Rashford, aliumaliza akiwa na mabao 30 na kukawa na matarajio makubwa kwake msimu huu lakini hali imekuwa tofauti, hadi sasa amefunga bao moja tu katika mechi 10.
Jumamosi iliyopita, Rashford alitolewa katika mechi dhidi ya Crystal Palace na nafasi yake kuingia kiungo Christian Eriksen wakati Man United ikihaha kusawazisha bao ililofungwa.
“Ukweli ni kuwa si mwenye kufunga kwa wakati huu lakini ana fursa, alipata nafasi tano au sita dhidi ya Brighton na kama angefanya juhudi angefunga, akiwekeza katika hilo kila siku na kuwa makini na kama wenzake watampa mipira na kumsaidia mambo yatakwenda,” alisema Ten Hag.
“Marcus Rashford ni mchezaji mwenye uwezo wa kufunga magoli katika kila mechi na anapokuwa katika eneo zuri atafunga,” alisema.
Kuhusu mwenendo usioridhisha wa timu yake, Ten Hag alisema, “timu inakwenda mbele lakini pia kuna mambo tunayotakiwa kuyaweka sawa, kuna mapungufu katika uchezaji wetu lakini hapo hapo kuna mambo chanya.”