Na mwandishi wetu
Baada ya Said Chino kufanikiwa kuibuka na ushindi wa TKO dhidi ya Mmalawi, Yobe Kamnyonya, bondia huyo amedai kuwa sasa anamuhitaji Ibrahim Mgenda ‘Ibra Class’ ili alipe kisasi.
Chino aliyasema hayo baada ya pambano hilo lililodumu kwa raundi tatu katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam jana Ijumaa huku Class aliyekuwepo ukumbini hapo naye akijibu mapigo kuwa Chino bado ana uwezo mdogo.
Wawili hao walipambana Mei, mwaka huu na Class kuibuka na ushindi wa pointi 98-91, 97-92, 97-92, hivyo Chino anahitaji pambano la marudiano ili mpinzani wake huyo athibitishe ubingwa wake.
Aidha, Chino alianza kwa kueleza kuwa ilibidi ashinde pambano lake dhidi ya Kamnyonya kwani alimzidi vitu vingi mpinzani wake huyo ikiwemo akili na nguvu, hivyo lilikuwa ni suala la muda tu.
“Kwa sasa nimeongezeka zaidi uzoefu na ninahitaji mabondia ambao mnawaona ni wakali, mfano Class ananikimbia kimbia sana, mara ya kwanza alishinda kwa pointi, nahitaji kukutana naye tena athibitishe ubingwa wake na akinipiga mara ya pili, mwenyewe nitakubali,” alisema Chino.
Class alisema: “Yaani Chino wa sasa namuona bado sana kwa kweli, nitampiga hata raundi ya tatu hatoboi na nina uhakika na hilo, mara ya kwanza nilimwonesha ngumi zinapigwa vipi akamaliza raundi lakini sasa hivi nasema ukweli hafiki raundi ya tatu.”