Na mwandishi wetu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars kwa kufuzu hatua inayofuata kuwania kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Wafcon) 2024 zitakazofanyika Morocco, mwakani.
Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Twiga ilishinda kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa ushindi wa 2-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliochezwa mjini Yamoussoukro, Ivory Coast, Twiga ilishinda mabao 2-0 na hivyo kulazimika kupigiana penalti.
“Pongezi kwa Twiga Stars kwa ushindi katika mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2024 kwa wanawake, dhidi ya Ivory Coast. Nawatakia kila la kheri katika hatua zinazofuata,” alisema.
“Kama nilivyoahidi, ushindi huu una zawadi ya motisha, Gerson Msigwa (Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo) utaratibu ule uendelee,” aliandika Rais Samia kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
Kutokana na ushindi huo, Rais Samia kupitia kwa Msigwa aliyehudhuria mchezo huo, alitoa kitita cha Sh milioni 10 kwa Twiga Stars kama pongezi kwa kusonga mbele.
Naye Kocha Mkuu wa Twiga, Bakari Shime alisema: “Mechi ilikuwa ngumu kwani tulikwenda mapumziko bila bao, lakini niwapongeze wachezaji kwani waliporudi kipindi cha pili walifunga mabao mawili kwa haraka haraka na kuwafanya wapinzani watoke mchezoni.”
Kwa ushindi huo Twiga sasa watacheza raundi ya mwisho na timu ya taifa ya Togo ambapo wakishinda watakuwa wamefuzu kwa mara ya pili kucheza Wafcon baada ya awali kushiriki mwaka 2010.
Soka Rais Samia aipongeza Twiga Stars
Rais Samia aipongeza Twiga Stars
Read also