Na mwandishi wetu
Tanzania imepanda nafasi mbili juu kutoka ya 124 hadi ya 122 kwenye viwango vya ubora vilivyotolewa mwezi Septemba, mwaka huu na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Viwango hivyo vilivyotolewa Alhamisi, vimekuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu baadhi ya timu kumaliza mechi za kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2023 na Tanzania ikiwa ni miongoni mwa timu zilizofanikiwa kufuzu.
Tanzania ilifuzu baada ya kutoka suluhu ugenini kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria na kufikisha pointi nane katika kundi lake nyuma ya vinara Algeria waliomaliza kwa pointi 16.
Katika kundi hilo, Uganda ilishika nafasi ya tatu kwa pointi saba na Niger ilishika mkia ikiambulia pointi mbili.
Pamoja na hayo, Ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda iko juu ikiwa katika nafasi ya 89 ikipanda nafasi tatu kutoka ya 92, ikifuatiwa na Kenya nafasi ya 106 iliyoshuka nafasi moja.
Kwa Afrika inayoongoza ni Morocco iliyo nafasi ya 13 ikipanda nafasi moja, Senegal ya 20 ikishuka nafasi mbili, Tunisia ya 29 ikipanda nafasi mbili, Algeria ya 34, Misri ya 35, Nigeria ya 40 zote zimeshuka kwa nafasi moja.
Mabingwa wa Kombe la Dunia, Argentina ndio kinara wa orodha ya jumla ikifuatiwa na Ufaransa, Brazil, England, Ubelgiji, Croatia, Uholanzi, Ureno, Italia na Hispania inayokamilisha kumi bora.
Kimataifa Tanzania yapanda viwango Fifa
Tanzania yapanda viwango Fifa
Read also