Na mwandishi wetu
Mfungaji wa bao pekee la Yanga katika mechi yao dhidi ya Namungo, Mudathir Yahya ameeleza kuwa kocha wake, Miguel Gamondi alimwekeleza nini cha kufanya ili wapate ushindi na alitekeleza alichoambiwa.
Mudathir aliyeingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya Pacome Zouzoua alifunga bao dakika ya 88 katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0 uliowarejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC.
“Mwalimu aliniambia kuwa wapinzani wamekaa nyuma kwenye lango lao hivyo ni ngumu kupata bao, akaniambia ukiona mpira umekwenda pembeni, nikimbie nyuma ya mabeki wa Namungo na kweli mpira ukapigwa krosi na Yao (Kouassi) nikafunga,” alisema Mudathir.
Kiungo huyo alifafanua kuwa kilichotokea kwenye bao hilo huwa wanajifunza kwenye uwanja wa mazoezi ndio maana walifanikiwa kupata ushindi japo si wa mabao 5-0 kama walivyofanya kwenye mechi zao mbili za awali za ligi msimu huu.
“Unajua wapinzani wakikaa nyuma mechi inakuwa ngumu sana, na nafasi tulitengeneza nyingi lakini walikuwa nyuma muda wote, endapo zile nafasi tungefunga mabao basi zingefika zile goli zetu (mabao 5-0) lakini haikuwa bahati tukafunga hilo moja,” alisema Mudathir.