Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Hispania aliyepigwa busu mdomoni, Jenni Hermoso hayumo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichotajwa hivi karibuni ingawa kocha mpya wa timu hiyo, Montse Tome amesema wako pamoja na mchezaji huyo.
Jenni alipigwa busu na aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales baada ya Hispania kubeba Kombe la Dunia kwa kuichapa England bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Agosti 20 mwaka huu.
Mchezaji huyo ameachwa katika timu hiyo ingawa wachezaji 21 kati ya 23 waliokuwa na timu ya Hispania iliyobeba Kombe la Dunia wamo katika kikosi hicho kipya.
Sakata la mchezaji huyo kupigwa busu lilimfanya Rubiales ajiuzulu licha ya awali kugoma kwa madai kwamba alimpiga busu mchezaji huyo baada ya kuwa na furaha isiyo kifani lakini baadaye alibadili uamuzi na kuamua kujiuzulu.
Kikosi hicho kilitangazwa Ijumaa iliyopita na kocha mpya wa timu hiyo, Montse Tome ambaye ni kocha wa kwanza mwanamke wa timu hiyo akichukua nafasi ya Jorge Vilda anayetajwa kuwa mshirika wa karibu wa Rubiales.
“Tuko pamoja na Jenni, tunaamini namna bora zaidi ya kumlinda ni kwa kufanya hivyo, Jenni ni mwenzetu, tunamtegemea,” alisema Tome.
Uteuzi wa timu hiyo umekuja huku kukiwa na mgomo wa wachezaji waliotangaza kutokuwa tayari kuichezea timu hiyo wakitaka Rubiales ajiuzulu pamoja na kufanyika mabadiliko ya ndani kwenye idara mbalimbali za REEF.
Baadaye REEF ilitoa taarifa ya kuwataka wachezaji hao kufuta mgomo huo na kuendelea kuichezea timu ya taifa watakapotakiwa kufanya hivyo.
Wachezaji wengine wanawake wa timu hiyo, Mapi Leon na Patri Guijarro wanaoichezea Barcelona ambao hawakuwamo katika kikosi cha Hispania kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia baada ya kuandika barua ya wazi ya kutotaka kufanya kazi chini ya kocha wa awali, Vilda nao wamo katika kikosi kipya.
Akizungumzia uamuzi wa kuwaita wachezaji hao, Tome alisema, “Ni mwanzo wa awamu mpya, muda unaenda mbele, hakuna kilicho nyuma yetu na hakika tunataka kuungana na wachezaji hawa.”
Hispania katika mechi za Nations Ligi itaumana na timu ya Sweden katika mechi itakayopigwa Septemba 22 na kufuatiwa na mechi nyingine dhidi ya Switzerland itakayopigwa Septemba 26.