Na mwandishi wetu
Yanga na Simba leo Jumamosi zimetupa karata zao za kwanza katika mechi za kwanza za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikitoka na ushindi wa mabao 2-0 na Simba ikiambulia sare ya mabao 2-2.
Timu hizo ambazo zote zilikuwa ugenini, Yanga ikiwa Rwanda kwenye Uwanja wa Pele ikiumana na Al Merreikh ya Sudan ambayo imeutumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani wakati Simba ilikuwa Zambia ikichuana na Power Daynamos.
Yanga ilipambana kwa kipindi chote cha kwanza bila kupata bao hata moja kabla ya kupata mabao yaliyofungwa na Kennedy Musonda dakika ya 62 na Clement Mzize dakika ya 79.
Kwa upande wa Simba mechi yao ilikuwa ngumu kwani dakika ya 30 ya mchezo Dynamos waliandika bao la kwanza lililofungwa na Joshua Mutale ambaye alionesha uwezo binafsi hadi kupata bao hilo.
Mutale aliambaa na mpira kwenye beki ya kulia ya Simba na kuuwahi wakati ukikaribia kutoka kabla ya kuurudisha uwanjani na kuipatia timu yake bao hilo pekee lililodumu kipindi chote cha kwanza.
Dakika 15 baada ya kuanza kipindi cha pili, Mwamba wa Lusaka, Clatous Chota Chama aliwainua vitini mashabiki wa Simba alipoipatia timu yake bao la kusawazisha lililotokana na shuti la Jean Baleke ambalo liliokolewa na kipa wa Dynamos kabla ya Chama kumalizia.

Kuingia kwa bao hilo kuliiongezea uhai Simba ambayo ililisakama lango la Dynamos na kumfanya kipa wa timu hiyo kufanya kazi ya ziada ya kuokoa mashambulizi hayo huku akiwalaumu mabeki wake kwa kuwaruhusu Simba kufika langoni mwao.
Katika dakika ya 70, Baleke alipoteza nafasi tatu ambazo angeweza kuipa Simba ushindi, mbili kati ya hizo zilionekana kuwaumiza mno mashabiki wa Simba pale alipopiga shuti dhaifu la juu wakati kipa akiwa tayari ametoka golini lakini kipa huyo kwa haraka alirudi na kuokoa mpira.
Nafasi ya pili, Baleke aliipoteza baada ya kuwa karibu na kipa wa Dynamos lakini shuti alilopiga liliokolewa na kipa huyo na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Katika hali ambayo haikutarajiwa Simba baada ya kushindwa kuzitumia nafasi hizo na nyinginezo walijikuta wakifungwa bao la pili mfungaji akiwa ni Cephas Mulombwa katika dakika ya 78.
Mulombwa alipiga shuti la chinichini ambalo kipa Ayoub Lankerd alishindwa kuuzuia mpira ambao ilionekana wazi kwamba angeweza kuudhibiti katika himaya yake.
Bao hilo hata hivyo halikuwakatisha tamaa Simba ambao waliendelea kulisakama mara kwa mara lango la Dynamos na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 90 baada ya Chama kufunga bao la kusawazisha kwa shuti kali la mguu wa kushoto.
Katika mechi hiyo, mwamuzi alimpa kadi nyekundu Dominic Chanda wa Dynamos baada ya kumshika Baleke ambaye alikuwa tayari amewatoka mabeki wa Dynamos akijiandaa kumkabili kipa wa timu hiyo.
Katika mechi hiyo kocha wa Simba, Robertinho Oliviera alifanya mabadiliko kadhaa akiwatoa Onana na nafasi yake kuchukuliwa na Saido Ntibazonkiza, pia alimtoa Dennis Kibu na kumuingiza Miquissone kabla ya kumtoa Mohamed Hussein na kumuingiza John Bocco.