Na mwandishi wetu
Msafara wa timu ya Yanga unatarajia kuondoka nchini kesho Alhamisi kuelekea Rwanda kwa ajili ya mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merreikh ya Sudan utakaopigwa Jumamosi hii, Uwanja wa Pele Kigali, Rwanda.
Jumla ya wachezaji 25 pamoja na viongozi 10 wa benchi la ufundi wanatarajiwa kuwemo kwenye msafara huo ambao utaondoka na Ndege ya Shirika la Air Tanzania majira ya mchana.
Habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo wachezaji wawili tegemezi kipa Djigui Diarra na kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki, wanatarajia kuungana na timu hiyo nchini Rwanda wakitokea nchini kwao walikokwenda kuzitumikia timu zao za taifa kuwania kufuzu fainali za Afcon.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema mpaka kufikia leo Jumatano hakuna mchezaji yeyote aliyekuwa majerahu na kurejea kwa Diarra na Aziz Ki kumeongeza matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo ambao wamepania kupata ushindi.
“Ni mchezo mgumu hilo halina ubishi hiyo inatokana na ubora waliokuwa nao Al Merreikh, lakini Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wenye uzoefu na mashindano haya, tunakwenda kucheza mpira wetu na kutafuta kile tulichokikusidia ambacho ni kuivusha timu hatua ya makundi,” alisema Gamondi.
Yanga imedhamiria kushinda na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuvunja rekodi mbaya ya kukaa miaka 25 bila kufika hatua hiyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.