Na mwandishi wetu
Kikosi cha timu ya Simba kinatarajia kuondoka kesho alhamisi asubuhi kuelekea Ndola, Zambia kwa ajili ya mechi yao ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos.
Simba imeeleza kuwa inaondoka na kikosi chake kamili baada ya leo Jumatano beki Henock Inonga kujiunga na timu hiyo huku Saido Ntibazonkiza akitarajiwa kujiunga na Wekundu hao nchini Zambia akirejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kila kitu kipo tayari, kinachosubiriwa ni safari kwa ajili ya kwenda kuianza vyema michuano hiyo ambayo Simba imeanza raundi ya kwanza na si ya awali kama ilivyoanza Dynamos.
Dynamos ilipenya hatua hiyo kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla ya sare ya mabao 2-2. Mechi ya ugenini dhidi ya African Stars ya Namibia, Dynamos ilifungwa mabao 2-1 kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
“Kila kitu kipo sawa, Inonga ameshaingia tayari na Saido atajiunga nasi kulekule Zambia, safari ya timu kutoka Dar es Salaam kwa usafiri wa ndege itaanza majira ya saa 4 asubuhi, kwa hiyo ratiba na mipango iko vizuri kabisa,” alisema Ally.
Ofisa huyo pia alisema kuwa mashabiki wa Wekundu hao wao wataanza safari ya kwenda kuishangilia timu hiyo katika mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola leo Jumatano majira ya saa 1.00 jioni kwa usafiri wa basi.
Alisema watasafiri usiku, wakitarajia kufika Tunduma kesho majira ya saa tano asubuhi na kupokelewa na Tawi la Wekundu wa Boda, kisha kufanya taratibu za uhamiaji kabla ya saa sita mchana kuanza safari ya kwenda Ndola.
“Tukifika Tunduma pamoja na yote tutafanya taratibu za kuvuka mpaka na kuanza safari ya kutembea na basi takriban kilometa 900 kuitafuta Ndola ambapo tunatarajia tutafika alhamisi (kesho) usiku,” alisema Ally.