Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema uzoefu wa wachezaji wake kwenye mashindano ya kimataifa unamfanya asiwe na hofu kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merreikh ya Sudan.
Msimu uliopita Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na USM Alger huku baadhi ya wachezaji wake wapya nao wakifika nusu fainali ya michuano hiyo hivyo wakionekana kuwa na uzoefu wa michuano hiyo.
Kocha huyo raia wa Argentina alisema pamoja na ugumu wa mchezo huo lakini anaamini kazi ya kuivusha timu hiyo kwenda hatua ya makundi haitokuwa ngumu kutokana na ubora na uzoefu waliokuwa nao wachezaji wake.
“Nina bahati kubwa wachezaji wangu wengi wana uzoefu na mashindano ya Caf, ukiachana na ubora ambao wanao, angalia kikosi changu ni wachezaji kama Max Nzengeli, Hafiz Konkoni, Gift Fred na Kibabage (Nickson) ndio unaweza kusema hawana uzoefu na mashindano ya Caf,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema imani hiyo haipo kwake tu bali hata wachezaji wake wanautamani mchezo huo kutokana na utayari waliokuwa nao pamoja na kiu ya kutaka kutimiza malengo ambayo wamekusudia kuyafikia kwenye michuano hiyo.
Alisema mbali ya kambi yao kuwa na shauku na mchezo huo wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo kuwania kuingia hatua ya makundi lakini kocha huyo amewataka wachezaji wake kutocheza na matokeo mfukoni.
Gamondi badala yake alisema kwamba wachezaji wake wanapaswa kupambana kwa dakika zote 90 za mchezo huo ili kuhakikisha wanaondoka na ushindi wakiwa ugenini.
Kikosi cha Yanga, kinatarajia kuondoa nchini keshokutwa Alhamisi kuelekea Rwanda ambako ndiko mchezo huo wa mkondo wa kwanza utachezwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Pele ambao Al Merreikh wameuchagua kuutumia katika mechi zao za nyumbani.