Na mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ (pichani) ameziomba Simba na Yanga kusaidiana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumanne kwenye uzinduzi wa Bodi ya Cosota na Bodi ya Filamu Tanzania, Mwinjuma alisema hata kama timu hizo zinashindwa kusaidiana kutokana na utamaduni wao basi wasihujumiane wala kuumizana.
Alisema amesikia malalamiko ya chini kwa chini kwamba timu hizo zinahujumiana akisema afadhali wafanyiane figisu katika michezo ya ndani lakini sio ya nje kwa kuwa wote wanakwenda kuwakilisha nchi, hivyo wanatamani kuona mafanikio yao.
“Tujue tunaenda kuwakilisha nchi hivyo kama kuna lolote linatokana na kuhujumiana liishe, sifikiri kama ni kitu sahihi kufanyiana hujuma hasa kwa timu za kimataifa,” alisema MwanaFA.
Naibu Waziri huyo alisema serikali inawategemea kufikia mafanikio ya juu zaidi ya walikotoka, wakajitahidi na kuzitakia kila la heri katika michezo yao itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii.
Yanga inatarajia kuondoka keshokutwa kuelekea Rwanda kwa ajili ya mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi hiyo dhidi ya Al Merreikh ya Sudan na Simba itacheza nchini Zambia dhidi ya Power Dynamos ya Zambia. Mechi zote zikitarajiwa kuchezwa Jumamosi hii.
Katika hatua hiyo, endapo timu hizo zitafanikiwa kuondoka na ushindi wa jumla, zitafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.