Rio de Janeiro, Brazil
Mshambuliaji wa Brazil, Neymar kwa sasa ndiye kinara wa wakati wote wa mabao wa timu ya taifa ya Brazil akiwa amempiku Pele kwa mabao mawili, Neymar sasa ana mabao 79.
Neymar ameweka rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili wakati Brazil ikiichapa Bolivia mabao 5-1 katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyopigwa usiku wa kuamkia leo Jumamosi.
Neymar alifunga mabao hayo mawili katika kipindi cha pili na huo ukiwa ni mchezo wake wa 125 katika timu ya Brazil ingawa tayari ametahadharisha kwamba yeye si bora kumzidi Pele.
“Sikuwahi kufikiria kuifikia rekodi hii, lakini mimi si bora kuliko Pele au mchezaji mwingine yeyote wa timu ya taifa,” alisema Neymar mchezaji wa zamani wa Barcelona na PSG ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Kwa kuvunja rekodi ya Pele Neymar amepewa tuzo maalum na shirikisho la soka la Brazil baada ya kuwa ndiye mwanasoka mwanaume anayeongoza kwa kuifungia Brazil mabao mengi kwa sasa.
Pele ambaye alifariki dunia Desemba mwaka jana akiwa na miaka 82, aliifungia Brazil mabao 77 katika mechi 92 kati ya mwaka 1957 hadi 1971 na hadi sasa anatajwa duniani kote kuwa mmoja wa wachezaji bora waliowahi kuuteka ulimwengu wa soka.
“Hongera kwako Neymar kwa kuipiku rekodi ya mfalme wa mabao wa Brazil, hata Pele naye pia anakupongeza kwa hili,” ilieleza taarifa ya shirikisho la soka Brazil.
Kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Fernando Diniz alisema: “Alikuja (Neymar) kufanya kile alichokifanya, alifunga mabao mawili na kuvunja rekodi.”