Sao Paulo, Brazil
Winga wa Manchester United, Antony ameondolewa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Brazil baada ya kuwapo tuhuma za udhalilishaji zilizotolewa na aliyekuwa rafiki yake wa kike.
Taarifa ya Shirikisho la Soka la Brazil ilieleza kuwa Antony, 23, ameondolewa katika kikosi hicho kwa kuwa kuna tuhuma zinazohitaji uchunguzi na tayari nafasi yake imejazwa na Gabriel Jesus wa Arsenal.
Timu ya Taifa ya Brazil inajiandaa kwa mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya timu za Bolivia na Peru.
Jana Jumatatu, tuhuma zinazomkabili, Antony zilichapishwa na chanzo kimoja cha habari nchini Brazil na tayari polisi wa majiji ya Manchester na Sao Paulo wameanza uchunguzi wa tuhuma hizo ambazo Antony amekana kuhusika.
“Naweza kusema kwamba tuhuma hizi ni za uwongo pamoja na ushahidi ambao tayari umewasilishwa, na ushahidi mwingine ambao utawasilishwa, sina kosa katika tuhuma ninazohusishwa nazo,” alisema Antony.
“Naamini uchunguzi unaoendelea kufanywa na polisi utaweka wazi ukweli kwamba sina kosa lolote,” aliongeza Antony.
Antony anadaiwa kumpiga kichwa hadi kumchana kichwani aliyekuwa rafiki yake wa kike, Gabriela Cavallin hadi kupelekwa hospitali kwa matibabu, tukio analodaiwa kulifanya Januari 15 wakati wakiwa katika chumba cha hoteli moja mjini Manchester.
Akizungumzia kipigo alichopewa, Gabriela alifafanua kuwa, Antony pia alimpiga ngumi kifuani na kwenye maziwa hadi kumuumiza hali ambayo inamfanya ahitaji operesheni ya kumuweka sawa.
Antony alikiri kuwa mahusiano yake na Gabriela hayakuwa mazuri lakini alisisitiza kwamba hakuwahi kumpiga kwa namna yoyote.
Klabu ya Manchester United ilikataa kuzungumzia tuhuma za Antony ikiwa ni siku chache baada ya mchezaji wao mwingine, Mason Greenwood kulazimika kuuzwa kwa mkopo katika klabu ya Getafe baada ya kukabiliwa na tuhuma za udhalilishaji kijinsia licha ya mahakama kumfutia tuhuma hizo.