London, England
Jopo la vigogo wa klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia limetua England kuishawishi Liverpool kwa mara ya mwisho ili ikubali kuwauzia mshambuliaji wao, Mohamed Salah kwa ada inayofikia Pauni 200 milioni kabla ya keshokutwa Alhamisi.
Alhamisi ndiyo siku ya mwisho kabla ya kufungwa rasmi kwa dirisha la usajili kwa ligi ya soka ya Saudi Arabia au Saudi Pro Ligi na kama Al-Ittihad itamkosa kabla ya siku hiyo mpango huo utakuwa umefeli.
Liverpool tayari imeshasema kwamba mshambuliaji huyo kutoka Misri ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 31 hauzwi, hiyo ni baada ya awali Al-Ittihad kumtangazia ofa ya Pauni 150 milioni.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp hataki kusikia habari ya Salah kuuzwa na kama akiuzwa mtu wa kwanza kukasirika atakuwa kocha huyo ambaye anaamini Salah ni mchezaji muhimu kwenye kikosi chake.
Juzi Jumapili, Salah aliifungia Liverpool bao wakati timu hiyo ikiibwaga Aston Villa 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu England huku Klopp akisema Salah amejidhatiti kuhakikisha anabaki Liverpool msimu huu.
Klopp pamoja na kutoa kauli hiyo lakini kinachoonekana ni kama vile hana uhakika wa asilimia 100 kwamba Salah ni lazima abaki Liverpool.
“Hakuniambia (kama anabaki) lakini hana sababu ya kuniambia hilo, kila kitu kinaonekana, ni kama anazungumza hilo mazoezini kwa kujituma kwake na tabia zake, tulikuwa na kikao wiki hii na kikao hakikuwa kuhusu tuliyoyafanya siku za nyuma bali kilihusu nini tutakifanya siku zijazo,” alisema Klopp.
Wakati hatma ya Salah ikiwa hivyo, mchezaji huyo tayari amewashuhudia wachezaji wenzake aliowahi kuwa nao Liverpool kina Fabinho, Roberto Firmino, Jordan Anderson na Sadio Mane wote wakitimkia Saudi Arabia.