Manchester, England
Winga wa Man United, Jadon Sancho amepingana na kocha wake, Erik ten Hag ambaye amesema kwamba alimuacha katika mechi waliyofungwa 3-1 na Arsenal kwa sababu alizembea mazoezini.
Sancho hata hivyo amepingana na Ten Hag akidai kwamba kocha huyo alichokisema ni kama amepata sababu ya kujivua lawama baada ya timu kufungwa.
Sancho, 23, aliachwa katika mechi hiyo na baada ya kipigo Ten Hag alisema kwamba walimuacha winga huyo kwa sababu alishindwa kufikia viwango katika mazoezi kabla ya mechi husika.
“Kutokana na kiwango chake kwenye mazoezi ndio maana hatukumchagua, hapa Manchester United ni lazima uwe kwenye kiwango kila siku, na kwa sababu hiyo katika mechi hii hakuchaguliwa,” alisema Ten Hag.
Muda mfupi baada ya Ten Hag kutoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandshi wa habari, Sancho alipingana naye kupitia mitandao ya kijamii akidai kwamba alichosema kocha huyo ni uwongo.
“Tafadhali msiamini kila kitu mnachokisoma, siwezi kuwaruhusu watu waseme mambo ambayo ni uwongo mtupu, nimekuwa nikijituma vizuri mazoezini katika wiki hii,” alisema Sancho.
Sancho badala yake alisema anaamini kuna sababu nyingine za matokeo hayo ambazo yeye asingeweza kuzizungumzia na kwamba kwa muda mrefu amekuwa akigeuzwa kisingizio jambo ambalo si haki.
“Kitu pekee ninachotaka kufanya ni kucheza mpira nikiwa mwenye tabasamu usoni na kuisaidia timu,” alisema Sancho.
Hii ni mara ya pili kwa Man United kupoteza mechi ya ligi msimu huu ikiwa tayari imeshapoteza mbele ya Tottenham kwa kuchapwa mabao 2-0.