Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Manchester United anayeandamwa na kashfa ya udhalilishaji kijinsia, Mason Greenwood amejiunga kwa mkopo na klabu ya Getafe inayoshiriki Ligi Kuu Hispania au La Liga.
Hatua hiyo imekuja baada ya mabosi wa Man United kutangaza kuwa mchezaji huyo angeondoka katika klabu hiyo kwa makubaliano maalum baada ya uchunguzi uliofanywa na klabu hiyo kwa miezi sita baada ya kufutiwa mashtaka ya kutaka kubaka na udhalilishaji kijinsia.
Greenwood, 21, mwezi Februari mwaka huu alifutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili lakini alijikuta katika wakati mgumu baada ya timu ya wanawake ya Man United na makundi ya wanaharakati kutishia kugoma na kuandamana iwapo mchezaji huyo angeruhusiwa kuichezea klabu hiyo.
“Hatua hiyo itamfanya Greenwood aanze kujenga upya maisha yake mapya ya soka nje ya klabu ya Manchester United. Klabu itaendelea kumpa sapoti Mason na familia yake katika kipindi hiki cha mpito,” ilieleza taarifa ya klabu ya Manchester United.
Getafe itakuwa ikilipa sehemu ndogo ya mshahara wa Greenwood ambaye bado ana mkataba na Man United unaofikia ukomo mwaka 2025.
Tangu ajiunge na Man United mwaka 2019 akiwa kijana wa miaka 17, Greenwood ameifungia timu hiyo mabao 35 katika mechi 129.
Greenwood hakuichezea Man United tangu Oktoba 2022 aliposhitakiwa kwa makosa ya kusudio la kubaka, ubabe na udhalilishaji kijinsia.
Mara baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani, makampuni ya Nike na Electronic Arts yalimfutia mchezaji huyo mikataba ya udhamini.