London, England
Kocha wa timu ya Taifa ya England, Gareth Southgate ametangaza kikosi chake kwa ajili ya mechi dhidi ya Ukraine na Scotland akiwajumuisha Jordan Henderson na Harry Maguire (pichani).
England itaumana na Ukraine Septemba 9 katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Ulaya au Euro 2024 ambayo itachezwa nchini Poland na Septemba 12 itacheza mechi ya kirafiki na Scotland.
Kiungo, Henderson, ameteuliwa baada ya kuondoka katika klabu ya Liverpool na kujiunga na Al-Ettifaq ya Saudi Arabia wakati Maguire amekuwa hana uhakika wa namba katika kikosi cha Man United na tayari amevuliwa unahodha wa timu hiyo.
Katika kikosi hicho Southgate pia amewaita kwa mara ya kwanza mshambuliaji wa Arsenal, Eddie Nketiah na beki wa kati wa Chelsea, Levi Colwill pamoja na kiungo wa Man City, Kalvin Phillips ingawa bado hajaanza kuichezea City.
Katika hatua nyingine, Southagate amemuacha katika kikosi hicho mshambuliaji wa Chelsea, Raheem Sterling akifanya hivyo kwa mara ya pili jambo ambalo linaibua hofu kuhusu majaliwa ya mchezaji huyo katika timu ya England.
“Sterling amekosekana kwa mara nyingine na ukweli ni kwamba hilo limewapa nafasi wengine kucheza vizuri na kujitengenezea mazingira katika timu, ni uteuzi mgumu na Raheem hajaufurahia lakini naamini atakuwa na msimu mzuri Chelsea, sina shaka kuhusu hilo,” alisema Southgate.
Kikosi kamili cha England na majina ya timu wanazotoka katika mabano ni kama ifuatavyo, makipa: Sam Johnstone (Crystal Palace), Jordan Pickford (Everton), Aaron Ramsdale (Arsenal)
Mabeki: Kieran Trippier (Newcastle), Kyle Walker (Man City) Ben Chilwell (Chelsea), Levi Colwill (Chelsea), Lewis Dunk (Brighton), Marc Guehi (Crystal Palace), Harry Maguire (Man United) na Fikayo Tomori (AC Milan),
Viungo: Trent Alexander-Arnold (Liverpool), Jude Bellingham (Real Madrid), Conor Gallagher (Chelsea), Jordan Henderson (Al-Ettifaq), Kalvin Phillips (Man City), Declan Rice (Arsenal)
Washambuliaji: Harry Kane (Bayern Munich), James Maddison (Tottenham), Eddie Nketiah (Arsenal), Marcus Rashford (Man United), Bukayo Saka (Arsenal), Callum Wilson (Newcastle), Eberechi Eze (Crystal Palace), Phil Foden (Man City) na Jack Grealish (Man City).