Na mwandishi wetu
JKT Queens ya Tanzania imefuzu kushiriki fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake baada ya kuilaza CBE ya Ethiopia kwa penalti 5-4 na kuibuka kinara wa michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Ushindi wa wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano hiyo ya Cecafa iliyofanyika nchini Uganda na kufikia tamati Jumatano hii, ulitokana na penalti za Ester Mabanza, Donisia Daniel, Winifrida Gerald, Happyness Hezron na nahodha wa timu hiyo Anastazia Antony.
Kwa upande wa CBE, timu inayomilikiwa na Benki ya Ethiopia, waliofunga penalti zao ni Loza Abera, Aregash Tadesse, Tinbit Samuel na Asfaw Emebet wakati aliyekosa ni Temesgen.
JKT Queens baada ya kuibuka kinara wa Cecafa sasa inajiandaa kwa fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazofanyika nchini Ivory Coast, kati ya Novemba 5 na 19 mwaka huu.
Katika dakika 90 za awali CBE walionesha uhai zaidi kwa kulisakama mara kadhaa lango la JKT lakini umahiri wa kipa Naijat Idriss ambaye ndiye aliyeibuka kipa bora wa michuano hiyo ulikuwa kikwazo kwa Waeethiopia hao kupata bao.
Mchezaji nyota wa CBE, Loza Abera mara mbili alikutana ana kwa ana na kipa wa JKT lakini Loza alishindwa kumchambua kipa huyo na kuzilamisha timu hizo kwenda katika dakika za nyongeza.
Shambulizi la kuogopesha ambalo JKT walilifanya katika lango la Ethiopia ni lile la kipindi cha pili lakini Donisia Daniel alishindwa kuitumia vizuri nafasi hiyo.
Mbali na Naijat aliyetwaa tuzo ya kipa bora mchezaji mwingine wa JKT aliyetwaa tuzo ni Stumai (MVP) wakati Fazila Ikwaput wa Kampala Queens alitwaa tuzo ya mfungaji bora akiwa na mabao manane na timu yake ilitwaa tuzo ya Fair Play.
Katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu, bao pekee la Lydia Akoth liliiwezesha Buja Queens ya Burundi kutoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Vihiga Queens ya Kenya.
Kimataifa JKT Queens yang’ara, Stumai ndiye MVP
JKT Queens yang’ara, Stumai ndiye MVP
Read also