Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kutoa dozi ya tano tano katika Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa JKT Tanzania 5-0 katika mechi iliyopigwa Jumanne hii usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Hii ni mechi ya tatu ya mashindano kwa Yanga kutoka na ushindi wa mabao matano na ya pili kwa Ligi Kuu NBC, matokeo yanayotoa picha ya namna mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo walivyojipanga kulitetea taji lao msimu huu.
Yanga tayari imefanya hivyo katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya KMC iliyoichapa 5-0 lakini pia imeipa kipigo cha 5-1 Asas ya Djibout katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ushindi dhidi ya JKT umeanza kuwapa jeuri mashabiki wa Yanga ambao katika vijiwe vyao wameanza kuitaja Simba kwamba ijiandae kukutana na dozi kama hiyo timu hizo zitakapokutana mapema mwezi Novemba.
Yanga sasa imefikisha pointi sita katika Ligi Kuu NBC sawa na Simba lakini Yanga inashika usukani ikiwa na faida ya mabao ya kufunga, ina mabao 10 wakati Simba ina mabao manne ikiwa nafasi ya tatu na Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na mabao sita, timu zote hizo zina pointi sita katika mechi mbili.
JKT licha ya kupewa kipigo kikali na Yanga, katika kipindi cha kwanza hawakuonesha dalili zozote za kukutana na kipigo kikubwa namna hiyo kwa jinsi walivyouanza mchezo wakijaribu kuzuia na kukabiliana na kasi ya Yanga.
Mambo hata hivyo yalianza kuwaaribikia mwishoni mwa kipindi cha kwanza walipoanza kupoteana na kumruhusu Stephanie Aziz Ki kuipatia Yanga bao la kwanza kwa mpira wa adhabu muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko.
Mambo yaliendelea kuwaharibikia JKT dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili walipofungwa bao la tatu mfungaji akiwa ni Nickson Kibabage.
Dakika 10 baada ya Kibabage kufunga bao la pili, JKT walijikuta wakiokota mpira katika nyavu zao kwa bao la tatu lililofungwa na Yao Kouasi.
Karamu ya mabao ya Yanga ilihimitishwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mabao mawili katika dakika za 79 na 88 na kukamilisha dozi ya mabao matano kwa Yanga.
Soka Yanga yaendeleza dozi ya tano tano
Yanga yaendeleza dozi ya tano tano
Read also