Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameomba uongozi umtafutie mechi mbili ngumu za kirafiki ili kuendelea kukiweka kwenye ushindani kikosi chake kabla ya kuivaa Power Dynamos kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Septemba 16, mwaka huu.
Simba ilikuwa na siku 30 za mapumziko lakini baada ya kumjua mpinzani wao kwenye michuano hiyo ya Afrika, Robertinho alisitisha mapumziko aliyowapa wachezaji na kutaka kuendelea na maandalizi kwa ajili ya kuwakabili mabingwa hao wa Zambia.
Dynamos imefika hapo baada ya kuiondosha African Stars ya Namibia kwa faida ya bao la ugenini ambapo Stars kwenye mechi ya nyumbani walishinda 2-1 kabla ya Dynamos kushinda kwao bao 1-0.
Kocha huyo raia wa Brazil alisema lengo la kuomba mechi za kirafiki ni kutaka kubaini mapungufu yao na ubora wa kimbinu wa wachezaji wake hasa ukizingatia wanakwenda kwenye mechi zinazohitaji umakini mkubwa ili kusonga mbele.
“Timu imecheza mechi mbili za ligi, kupata mapumziko ni kujirudisha nyuma hasa ikizingatiwa tunakabiliwa na mchezo mgumu wa kufuzu hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, tunahitaji kuwa na mazoezi mepesi na ya nguvu, lengo ni kuitengeneza timu ya ushindani ndani ya dakika zote 90 haitakuwa rahisi kama tutafanya mazoezi bila mechi za kirafiki,” alisema Robertinho.
Robertinho alisema hajui ni timu gani ambazo uongozi utampatia lakini angependa kucheza na timu zenye kiwango cha Simba zitakazowapa changamoto wachezaji wake na kuwajengea utimamu, ari ya upambanaji na pumzi ili wahimili presha kutoka kwa wapinzani.
Alisema kwa hapa Tanzania akiipata Azam FC au Singida Foutain Gate itakuwa nzuri lakini hata ikitokea akipata timu kutoka nje ya Tanzania ni jambo jema kwani atakuwa amepata kipimo sahihi kuelekea mchezo huo dhidi ya Dynamos.
Simba ni kati ya timu 10 za Afrika zilizopangwa kuanza kampeni ya kusaka taji la Ligi ya Mabingwa raundi ya kwanza, timu nyingine ni Al Ahly, Wydad CA, Horoya AC, Mamelodi Sundwons, Petro de Luanda, Esperance, TP Mazembe, Pyramids na CR Belouizdad.