Na mwandishi wetu
Klabu ya JS Kabylie ya Algeria imemtambulisha rasmi mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Simon Msuva kujiunga na kikosi chao kwa mkataba wa miaka miwili.
Kabylie inayoshiriki Ligi Kuu Algeria maarufu Division 1 imekamilisha dili hilo baada ya mchuano mkali wa kuwania saini ya mshambuliaji huyo dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo, CR Belouizdad.
Kabylie ambao walitolewa hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na ES Tunis, imemtangaza Msuva leo Jumanne kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii akiwa ni mchezaji wa 12 kumsajili katika dirisha kubwa la usajili mpaka sasa.
“Usajili majira ya joto sokoni msimu wa 2023-24 usajili wa 12: mchezaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva mwenye miaka 29, amejiunga na JSK kwa mkataba wa miaka miwili,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa zaidi hata hivyo zinafafanua kuwa Msuva amekataa ofa ya kujiunga na Beloizdad inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck kutokana na kuvutiwa na maono ya Kabylie iliyomaliza nafasi ya 14 kwenye Division 1 msimu uliopita.
Msuva aliyemaliza mkataba wake na Al-Qadsiah ya Saudi Arabia msimu uliopita alikuwa akitajwa pia kuwaniwa na vigogo wa Tanzania, Simba na Yanga lakini tangu awali mchezaji huyo aliyewahi kukipiga Wydad AC na Difaa El Jadida aliweka wazi kutohitaji kurejea kucheza soka Tanzania kwa sasa.
Kimataifa Msuva asaini JS Kabylie
Msuva asaini JS Kabylie
Read also