Na mwandishi wetu, kampala
JKT Queens imetinga fainali ya michuano ya Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa wanawake na sasa itaumana na CBE FC ya Ethiopia, mechi itakayopigwa Jumatano hii.
Mshindi wa mechi hiyo mbali na kuwa bingwa wa michuano hiyo lakini pia atakuwa amejikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake, michuano itakayofanyika nchini Ivory Coast.
JKT Queens imefuzu hatua hiyo kwa kuilaza Buja Queens ya Burundi mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali ya kwanza wakati CBE ilifuzu kwa kuichapa Vihiga Queens mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya pili, mechi zote hizo zilichezwa Jumapili hii.
JKT Queens ambao hadi sasa hawajapoteza hata mechi moja, katika mechi na Buja Queens, walikuwa wa kwanza kufungwa kwa bao la dakika ya 11 mfungaji akiwa Toepistar Situma.
Bao hilo halikuwakatisha tamaa JKT Queens ambao walizinduka kipindi cha pili wakineemeka kwa mabao ya Donisia Minja dakika ya 63, Stumai Abdallah dakika ya 76 na Winfrida Gerald dakika za majeruhi.
Kwa upande wa CBE, nao ndio waliokuwa wa kwanza kufungwa bao na Bertha Omita wa Vihiga katika dakika ya 10 lakini walisawazisha katika dakika za nyongeza kupitia kwa nahodha wao Loza Abera na kufanya matokeo yawe sare ya 1-1 na timu hizo kuongezewa dakika 30.
CBE walizitumia vizuri dakika 30 na kufunga bao pekee na la ushindi lililowapeleka fainali mfungaji akiwa ni Aregash Tadesse.
Kabla ya mechi ya fainali ya JKT na CBE, Buja na Vihiga wataumana mapema katika mechi ya kusaka nafasi ya tatu.
Kimataifa JKT Queens yatinga fainali Cecafa, kuivaa CBE
JKT Queens yatinga fainali Cecafa, kuivaa CBE
Read also