Na mwandishi wetu
Yanga imeianza Ligi Kuu NBC kwa kishindo na kutoa onyo kwa timu nyingine baada ya kuilaza KMC mabao 5-0 katika mechi iliyopigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Ushindi huo katika mechi ya kwanza ya timu hiyo utaifanya KMC ijiulize mara mbili kwani licha ya kunyanyaswa mara kadhaa na Yanga lakini haijawahi kufungwa mabao mengi namna hiyo tangu ipande ligi kuu mwaka 2018.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi, walipata bao lao la kwanza katika dakika ya 17 mfungaji akiwa ni Dickson Job ambaye aliupiga kwa kisigino mpira uliotokana na krosi ya Aziz K kabla ya kuokolewa na kipa wa KMC, Wilbol Maseke na kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.
Kuingia kwa bao hilo hakukutoa dalili zozote za KMC kufungwa mabao mengi licha ya Yanga kutengeneza nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia lakini hadi timu zinakwenda mapumziko, Yanga ilikuwa mbele kwa bao hilo pekee.
Dakika 13 baada ya kuanza kipindi cha pili, Yanga iliandika bao la pili mfungaji akiwa ni Aziz Ki ambaye aliunganishiwa mpira na Moloko huku KMC wakishindwa kutema cheche katika lango la Yanga lililolindwa na kipa Metacha Mnata.
Kuingia kwa Hafiz Konkoni akichukua nafasi ya Kennedy Musonda kulizaa bao la tatu la Yanga lililofungwa na mchezaji huyo dakika ya 69 ambaye aliuwahi mpira wa adhabu uliopigwa na Aziz Ki na kutokea piga nikupige langoni mwa KMC kabla ya mpira kumkuta mfungaji.
Kipa wa KMC, Maseke awali aliokoa mpira huo lakini mwamuzi akaipa Yanga bao kwa kuwa mpira uliookolewa na kipa huyo ulikuwa tayari umevuka mstari.
Bao la nne la Yanga lilifungwa na Mudathir Yahya katika dakika ya 77 akiutumia mpira uliotoka kwa Konkoni ambaye alimpora beki mmoja wa KMC.
Karamu ya mabao ya Yanga ilihitimishwa katika dakika ya 81 kwa bao lililofungwa na Pacome ambaye aliitumia vizuri pasi ya Maxi Nzengeli.
Ushindi huo unaifanya Yanga kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tatu na mabao matano na imecheza mechi moja ikiwa imezidiwa pointi tatu na Simba inayoshika usukani ikiwa imecheza mechi mbili na ina mabao sita ya kufunga.
Hadi sasa Feisal Salum au Fei Toto wa Azam FC ndiye anayeongoza kwa kuwa na mabao mengi katika ligi hiyo akifuatiwa na Jean Baleke wa Simba na Mateo Anthony wa Mtibwa wenye mabao mawili kila mmoja.
Soka Yanga yaanza ligi kwa kishindo
Yanga yaanza ligi kwa kishindo
Read also