Manchester, England
Klabu ya Manchester City imethibitisha kuwa kocha wake, Pep Guardiola atazikosa mechi kadhaa za timu hiyo baada ya kufanyiwa operesheni ya mgongo.
Pep ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 52, jana Jumanne alifanyiwa upasuaji huo mjini Barcelona na hivyo atazikosa mechi mbili za timu hiyo dhidi ya Sheffield United na dhidi ya Fulham wakati akiendelea kujiuguza.
Katika kipindi hicho nafasi ya Pep itashikwa na mmoja wa wasaidizi wake, Juanma Lillo, kazi ambayo ataifanya hadi kocha huyo atakapopona na kurejea kazini. Pep anatarajia kurudi kazini Septemba 16.
“Kocha wa Manchester City amekuwa na matatizo ya mgongo kwa kipindi kirefu sasa na mwishowe alisafiri hadi Barcelona kwa ajili ya kufanyiwa operesheni ambayo imefanywa kwa mafanikio na ataendelea kuwa Barcelona akijiuguza hadi kupona,” ilieleza taarifa ya Man City.
“Kila mmoja hapa Manchester City anamtakia kila lakheri Pep apone na tunasubiri kwa hamu kumuona akirudi haraka Manchester,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Man City imezianza mbio za msimu mpya wa 2023-24 kwa ushindi wa mechi zake mbili za kwanza dhidi ya Burnley na Newcastle lakini pia imefanikiwa kulibeba taji la Uefa Super Cup baada ya kuilaza Sevilla kwa mikwaju ya penalti 5-4.
Kimataifa Pep afanyiwa operesheni ya mgongo
Pep afanyiwa operesheni ya mgongo
Read also