Madrid, Hispania
Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez amekerwa na kitendo cha kiongozi wa Shirkisho la Soka Hispania (RFEF), Luis Rubiales kumpiga busu mdomoni mchezaji wa timu hiyo, Jernni Hermoso akisema kwamba msamaha alioomba kiongozi huyo hautoshi.
Mara baada ya Hispania kuifunga England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) Jumapili iliyopita, Rubialles alimpiga Jenni busu mdomoni lakini baada ya kushutumiwa kila kona, juzi aliibuka na kuomba msamaha akidai alikosea.
Awali Rubiales aliwashangaa waliokuwa wakimshutumu akisema kuwa alichokifanya kilitokana na furaha aliyokuwa nayo na kwamba tukio hilo lilikuwa la marafiki wawili akitaka waliolipa tafsiri nyingine wapuuzwe.
“Tulichokiona ni kitu kisichokubalika, hatua ya Rubiales kuomba msamaha haitoshi na nafikiri ni kitu ambacho hakikubaliki, anatakiwa kuchukua hatua zaidi ili kuweka wazi kitu ambacho sote tulikiona,” alisema Waziri Mkuu Sanchez.
“Wachezaji walifanya kila walichoweza ili kupata ushindi lakini tabia aliyoionesha Rubiales imetoa picha ya wazi kwamba bado kuna kazi ya kufanya katika kuekelea kwenye usawa,” alisema Waziri Sanchez.
Naye Waziri Mkuu wa Pili wa Hispania, Yolanda Diaz, yeye alimtaka Rubiales ajiuzulu katika nafasi yake kwenye kuongoza RFEF.
“Msamaha anaoomba hauna maana, kikosi cha Hispania kimetuonesha mambo mengi kuhusu usawa, si katika michezo na soka tu, wametuonesha kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika nchi yetu ili wanawake na wanaume wawe sawa,” alisema Waziri Diaz.
Awali kupitia mtandao wa Instagram, Jenni alisema hakupenda alichofanyiwa na Rubiales baada ya mechi yao ya fainali lakini taarifa iliyotolewa baadaye ilimnukuu mchezaji huo akimtetea Rubiales.
Mbali na mawaziri hao wawili, Rubiales pia ameshutumiwa na mawaziri wengine pamoja na watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii huku wengine wakimtaka ajiuzulu.
Katika kauli yake ya kuomba msamaha, Rubiales alisema, “Nalazimika kuomba msamaha na kujifunza kupitia jambo hili na kuelewa kwamba unapokuwa rais ni lazima kuwa makini.”