Na mwandishi wetu
Yanga imeanza na mguu mzuri michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuilaza ya Asas ya Djibout mabao 2-0 wakati Azam ikilala kwa mabao 2-1 mbele ya Kanema ya Ethiopia.
Katika mechi hizo zilizochezwa Jumapili hii, Yanga wakiwa Uwanja wa Azam Complex walianza kuhesabu bao la kwanza dakika ya 22 mfungaji akiwa ni Aziz Ki kwa shuti la chinichini akiitumia pasi ya Lomalisa Mutambala
Yanga ambao walikuwa wageni wa mchezo huo baada ya Asas kuutumia uwanja wa Azam kama uwanja wa nyumbani, waliandika bao la pili dakika ya 53 likifungwa na Kennedy Musonda.
Yanga hata hivyo itabidi wajilaumu kwa kushindwa kuzitumia nafasi nyingi walizotengeneza jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi ya marudiano na nyinginezo iwapo timu hiyo itasonga mbele.
Katika mechi hiyo, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa kipindi cha pili akiwaingiza Salum Aboubakar, Pacome Zouazoua, Jesus Moloko, Hafiz Konkoni na Farid Mussa kuchukua nafasi za Khalid Aucho, Clement Mzize, Maxi Nzengeli, Musonda na Lomalisa.
Kwa upande wa Azam FC iliyokuwa ugenini Ethiopia, ilijikuta ikichapwa bao la kwanza dakika ya 21 ya mchezo huo baada ya kipa wake, Idrissu Abdilah kujaribu kuumiliki mpira kifuani lakini hesabu zikakataa na mpira huo kunaswa na mchezaji wa Kanema, Fitsum Tilahun ambaye aliujaza wavuni kiulaini kwenye lango lililokuwa tupu.

Azam FC licha ya kupambana ikisaka bao la kusawazisha, ilijikuta ikichapwa bao la pili dakika ya 61 lililofungwa na Tilahun aliyemchungulia kipa wa Azam na kuupiga mpira uliokwenda hadi wavuni.
Bao pekee la kufutia machozi la Azam FC lilipatikana katika dakika ya 73 mfungaji akiwa ni Idriss Mbombo ambaye aliingia akitokea benchi.
Ili iweze kusonga mbele, Azam sasa itakuwa na kazi ya kuhakikisha inapata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano itakayochezwa Dar es Salaam wiki moja ijayo.