Na mwandishi wetu
Kiu ya mashabiki wa Simba kumuona mshambuliaji wao, Moses Phiri akizifumania nyavu imetimia Jumapili hii baada ya kufunga bao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Phiri alikuwa tishio kwa mabao msimu uliopita kiasi cha kuonekana kama angetishia himaya ya Fiston Mayele wa Yanga katika kuzifumania nyavu kabla ya kuumia Desemba mwaka jana.
Baada ya kuumia, Phiri alikosa mechi zote zilizobaki za msimu huo kabla ya kupona hivi karibuni lakini kocha wa Simba, Robertinho, amekuwa akimuweka benchi hadi baadhi ya mashabiki kuhoji ni kwa nini hapewi nafasi.
Bao la Phiri ambalo ni la kwanza msimu huu, lilipokewa kwa shangwe na mashabiki wa Simba waliofurika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam pengine wakiamini mkali wao wa mabao, kwa mara nyingine ameanza kuonesha makali waliyoyakosa kwa kipindi kirefu.
Simba iliandika bao lake la kwanza dakika mbili kabla ya mapumziko mfungaji akiwa ni Jean Baleke ambaye aliitumia vizuri krosi ya beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Simba ikiwa mbele.
Phiri ambaye aliingia kipindi cha pili pamoja na Luis Miquissone baada ya kutolewa Willy Onana na Baleke, alifunga bao lake dakika ya 55 akiitumia vizuri pasi ya beki wa kulia wa Simba, Shomary Kapombe.
Kwa ushindi huo, Simba sasa inashika usukani wa ligi ikiwa imefikisha pointi sita na mabao sita ya kufunga ikiwa imefungwa mabao mawili.
Soka Phiri aanza kutupia Dar
Phiri aanza kutupia Dar
Read also