Madrid, Hispania
Rais wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales ameshutumiwa kwa kumpiga busu ‘zito’ mchezaji wa timu ya Hispania Jenni Hermoso wakati akifurahia Hispania kubeba Kombe la Dunia la Wanawake.
Hispania jana Jumapili iliichapa England bao 1-0 na kubeba kombe hilo ikineemeka kwa bao hilo pekee lililofungwa na nahodha wa timu hiyo, Olga Carmona katika dakika ya 29 ya mchezo huo.
Rubiales alimpiga busu Jenni katika hafla ya kukabidhiwa tuzo ya ushindi akionekana mwenye furaha lakini jinsi alivyofanya jambo hilo ni kitu kilichoibua mshangao na kiongozi huyo kujikuta akishutumiwa kila kona huku, Jenni mwenyewe akisema hakupenda alichofanyiwa.
“Sikupenda,” alisema Jenni kupitia mitandao ya kijamii lakini baadaye taarifa ya shirikisho ilimtetea rais huyo wa soka kwa alichokifanya japo viongozi kadhaa waandamizi wa serikali walimshutumu.
Waziri wa Haki na Usawa wa Hispania, Irene Montero alisema kwamba alichofanya Rubiales ni aina nyingine ya udhalilishaji kijinsia dhidi ya wanawake.
“Hii nayo ni aina ya udhalilishaji kijinsia ambayo wanawake wanakutana nayo katika maisha yao ya kila siku, ni jambo ambalo hatuwezi kulichukulia kuwa la kawaida tu,” alisema.
“Tunawajibika kutojenga dhana kwamba kumpiga mtu busu bila ridhaa yake ni jambo ambalo linatokea tu hivi hivi,” alisema.
Baadaye katika taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka, Jenni mwenye umri wa miaka 31 anadaiwa kusema kwamba busu hilo lilitokana na furaha iliyopitiliza ya kushinda Kombe la Dunia na ni jambo la kawaida kutokea.

Busu hilo limemfanya Rubiales kushutumiwa kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya waliotoa maoni hasa kupitia mtandao wa Twitter au X wakimtaka kiongozi huyo kujiuzulu.
Rubiales alizungumza na redio moja akidai kwamba busu hilo ni baina ya marafiki wawili wanaofurahia jambo fulani, na wanaoliangalia kwa namna tofauti ni watu wajinga na wa hovyo. “Tuwapuuze na tuendelee kufurahia mambo mazuri.”
Gazeti la El Pais la Hispania lilitoka na kichwa cha habari kikubwa kilichosena, ‘Jenni hakupenda busu la Rubiales, na sisi hatukupenda.”