Na mwandishi wetu
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo (pichani) amesema bodi hiyo pamoja na TFF, hawahusiki katika sakata la timu ya Kitayosce kushindwa kutumia wachezaji wake wapya iliyowasajili kwenye dirisha kubwa msimu huu bali ni uzembe wa viongozi wa timu hiyo.
Jana timu hiyo ilijikuta ikicheza pungufu ikiwa na wachezaji wanane uwanjani katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Azam FC na kufungwa mabao 4-0.
Mchezo huo hata hivyo ulivunjika baada ya wachezaji wawili wa timu hiyo akiwemo kipa kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kasongo alisema awali timu hiyo ilifungiwa kufanya usajili na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), baada ya kupitisha siku 45 bila kumlipa mchezaji ambaye alikwenda kuwashitaki wakati wakiwa wanashiriki Ligi ya Champioship msimu uliopita.
Alisema taarifa za Kitayosce kufungiwa walipewa na Fifa siku moja kabla ya timu hiyo kupambana na Azam na walichofanya wao waliifahamisha timu hiyo na kitu kizuri viongozi wa timu hiyo walipambana na kumlipa mchezaji huyo na Fifa ikawaondolea kifungo hicho.
“Adhabu ya Fifa haihusiani na hiki ambacho viongozi wa Kitayosce wamekifanya, viongozi hao wameshindwa kuwalipia vibali vya kufanya kazi nchini wachezaji 12 wa kigeni lakini Bodi ya Ligi wala TFF hawahusiki katika hili, wazembe ni viongozi sababu sisi kama bodi tangu asubuhi ya siku ya mchezo tulikuwa tunawauliza na majibu yao yalikuwa tumekamilisha kila kitu,” alisema Kasongo.
Kauli ya Kasongo imeungwa mkono na aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini na Katibu Mkuu wa FAT (sasa TFF), Ismail Aden Rage ambaye alisema viongozi wa timu hiyo wanahusika kwa kiasi kikubwa kwa uzembe walioufanya wa kushindwa kuwatafutia vibali wachezaji wao wa kigeni.
Rage alisema wamemkera sababu siku mbili nyuma kabla ya mchezo dhidi ya Azam alikuwa akiwapigia simu kuwauliza kama wana tatizo lolote lakini walijibu wako sawa.
Alisema kwamba juzi asubuhi viongozi hao walimpigia simu wakamwomba afike uwanjani kushuhudia mchezo wao lakini ameambulia fedheha kwa timu ya nyumbani kwao Tabora kucheza pungufu kwa uzembe wa viongozi.
“Sheria walizochukua waamuzi ni stahiki kabisa sababu huwezi kuendelea na mchezo ukiwa na wachezaji sita, kifupi wamenikera hawa viongozi wa hii timu sijawahi kwenda Uwanja wa Azam, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza lakini wameniaibisha,” alisema Rage.
Soka TFF yajivua lawama kwa Kitayosce
TFF yajivua lawama kwa Kitayosce
Read also