Na mwandishi wetu
Timu ya Kitayosce ya Tabora ni kama vile imekuwa na misukosuko mikubwa tangu imalize kampeni za kupanda Ligi Kuu NBC msimu huu, kitendo kilichopelekea matokeo mabovu na aibu katika mchezo wao wa kwanza wa ligi hiyo.
Julai, mwaka huu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza timu hiyo kufungiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa kilichoelezwa kutomlipa stahiki zake kocha Ahmed Soliman raia wa Misri.
Baadae ilimalizana na kocha huyo na kuachiwa huru, lakini siku mbili kabla ya mechi yao ya kwanza ya ligi dhidi ya Azam FC, TFF ikaikumbusha timu hiyo kuwasilisha majina ya usajili wa wachezaji wao katika mtandao wa Fifa.
Kama hiyo haitoshi, jana siku ya mchezo wenyewe Kitayosce ambayo imeeleza kubadili jina lake na kuitwa Tabora United, ilifungiwa kwa mara nyingine kufanya usajili kutokana na madai ya kumvunjia mkataba mchezaji wa Ghana, Rahim Osumanu na kutomlipa stahiki zake.
Lakini baadae TFF kwa mara nyingine ikaeleza kuwa Kitayosce imelimaliza suala hilo lakini ikawa na changamoto ya kutokamilisha taratibu za kuwatumia wachezaji wake katika ligi kuu na hivyo kuanza na wachezaji wanane pekee katika mechi yao hiyo iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Benchi lao la ufundi lilikuwa na kocha msaidizi, Bernard Fabian pekee, hiyo ni kutokana na makocha wa timu hiyo akiwemo kocha mkuu kutoka Serbia, Goran Kopunovic kukosa vigezo vya kuwepo katika benchi hilo.
Katika mechi hiyo, mpaka dakika ya 13 tayari Kitayose ilishafungwa mabao manne kabla ya wachezaji wake wawili kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo na hivyo mechi hiyo kumalizwa kwa mujibu wa kanuni.
Inaruhusiwa timu kuanza mechi ikiwa na wachezaji wasiopungua saba, hivyo kutoendelea kwa wachezaji hao kulifanya wabaki sita uwanjani na hivyo mwamuzi kumaliza mechi hiyo dakika ya 15.
Soka Majanga ya Kitayosce mwanzo mwisho
Majanga ya Kitayosce mwanzo mwisho
Read also