Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imesema kuwa beki wa kati wa timu hiyo, Henock Inonga atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili sawa na siku 14 akiuguza jeraha lake la bega.
Daktari wa timu hiyo, Edwin Kagabo alifafanua kuwa mchezaji huyo hajapata majeraha makubwa kama ilivyodhaniwa baada ya kuumia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate iliyopigwa wiki iliyopita, hivyo atakaa nje kwa muda huo kisha atarejea kazini.
“Kulingana na vipimo baada ya kumchunguza zaidi, imeonekana Inonga hajapata madhara makubwa kama ambavyo pengine ilihisiwa, hivyo atakaa nje akiuguza jeraha hilo ili kuwa kamili kabisa kabla ya kurejea uwanjani rasmi,” alisema Kagabo.
Inonga aliumia kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kukosekana kwenye mechi ya fainali ya Ngao ambapo Simba walishinda kwa matuta 3-1 baada ya suluhu ya dakika 90 za kawaida.
Beki huyo ataukosa pia mchezo wa awali wa Ligi Kuu NBC wa kesho ambapo Simba itaanza ligi kwa kuumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro kuanzia saa 10 jioni.
Soka Inonga nje wiki mbili
Inonga nje wiki mbili
Read also