Na mwandishi wetu
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Karim Mandoga ‘Mtu Kazi’, (pichani) ataendelea kupanda ulingoni baada ya vipimo alivyofanyiwa jana Jumatatu kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukutwa hana tatizo lolote.
Awali ilielezwa kuwa bondia huyo alipaswa kufanyiwa vipimo kwanza kabla ya kuendelea na pambano jingine baada ya kupoteza kwa TKO dhidi ya Moses Golola wa Uganda katika pambano la raundi nane lililofanyika Julai 29, mwaka huu Jijini Mwanza.
Na kama ingebainika kuwa na tatizo kutokana na matokeo hayo ya Mwanza, basi Mandonga angefungiwa kwa kipindi cha wiki sita kupanda ulingoni mpaka hapo baadae.
Meneja wa Mandonga, Ally Rashid alisema leo Jumanne kuwa bondia wake atapanda ulingoni Agosti 27, visiwani Zanzibar baada ya majibu ya vipimo alivyofanyiwa kuonesha hana tatizo lolote la kumfanya ashindwe kupambana.
“Vipimo vimeonesha Mandonga yupo fiti na ameruhusiwa kupanda ulingoni kwenye pambano la Agosti 27, kwa sasa tunaendelea na maandalizi kama ilivyokuwa awali kabla ya taarifa za kutakiwa kufanya vipimo, tuna imani mashabiki wetu watakuja kwa wingi ili kuona Mtu Kazi akirudisha heshima yake baada ya hivi karibuni kupoteza mapambano mawili mfululizo,” alisema Rashid.
Awali Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) ilieleza kuwa wanafikiria kumfanyia vipimo vya afya bondia huyo kama sheria za kimataifa za mchezo huo zinavyoeleza na kama angekutwa na tatizo angezuiwa kupanda ulingoni Agosti 27.
Mwezi uliopita Mandonga alipanda ulingoni mara mbili kwenye mapambano mawili tofauti, miongoni mwao alilopigana Kenya na kupoteza kwa KO dhidi ya Danny Wanyoni kabla ya kuchapwa tena mjini Mwanza.
Ngumi Vipimo vyamruhusu Mandonga kupanda ulingoni
Vipimo vyamruhusu Mandonga kupanda ulingoni
Read also