Na mwandishi wetu
Timu ya JKT Queens kesho Jumatano inashuka Uwanja wa Omondi, Kampala kukipiga na New Generation ya Zanzibar katika mchezo wa pili wa michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cacafa).
Mshauri wa benchi la ufundi la JKT, Bakari Shime alisema anaamini wataondoka na pointi tatu dhidi ya Generation ili wasonge hatua inayofuata kwa kuwa lengo lao ni kufika fainali na kuchukua ubingwa.
“Kwa upande wetu kwanza tumeona ugumu ukoje na kazi yetu ni kuangalia tathmini ya mashindano yote ili kuona timu yetu inajipanga zaidi namna gani kufika fainali na kisha kuchukua ubingwa, naamini tutafanikiwa kesho kuchukua alama ambazo zitatupeleka hatua nyingine,” alisema Shime.
Naye Kocha Mkuu wa Generation, Ramadhani Abdulrahman alisema: “Wachezaji wako vizuri lakini mechi ya kwanza tulipoteza kutokana na kuruhusu bao la pili ambalo liliwavunja moyo sababu bado wadogo kwa hiyo tunajipanga kuhakikisha tunashinda mechi yetu na JKT,” alisema.
Katika michuano hiyo inayofanyika nchini Uganda, JKT ilishinda mchezo wake wa kwanza dhidi ya AS Kigali ya Rwanda kwa mabao 2-1 wakati Generation ilifungwa mabao 3-1 na Vihiga Queens ya Kenya.
Bingwa wa michuano hiyo atakata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajia kufanyika Ivory Coast ambapo bingwa mtetezi wa mashindano hayo ni FAR Rabat ya Morocco.
Soka JKT Queens, New Generation uwanjani
JKT Queens, New Generation uwanjani
Read also