Na mwandishi wetu
Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said ameahidi kutoa Sh milioni 200, kwa wachezaji na benchi la ufundi endapo watashinda mchezo wa fainali wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao Simba SC.
Mchezo huo wa fainali unatarajia kuchezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuanzia saa moja jioni na hiyo ni baada ya timu hizo kuibuka washindi katika mechi za nusu fainali.
Yanga iliifunga Azam mabao 2-0 wakati Simba iliiondosha Singida Fountain Gate kwa penalti 4-2 baada ya matokeo ya suluhu kwenye dakika 90 za awali.
Akizungumza na mtandao wa timu hiyo, Hersi alisema ameamua kutoa ofa hiyo kama hamasa kwa wachezaji wake ili wazidi kujituma na kulitetea taji hilo ambalo wanalishikilia kwa mara ya pili mfululizo.
“Uongozi kwa pamoja tumekubaliana kutoa ofa hiyo kwa wachezaji wetu nadhani hiyo itawaongezea hamasa hata wachezaji wageni na kuzidi kujituma kwa ajili ya kuipigania timu na maslahi yao kwa ujumla,” alisema Hersi.
Kiongozi huyo alisema mpaka sasa wanafurahishwa na mwanzo mzuri wa benchi lao jipya la ufundi chini ya kocha Miguel Gamondi na wasaidizi wake na imani yao ni kwamba ubora wanaouonesha kwenye mechi hizo za Ngao ya Jamii hautoishia hapo.
Alisema wao kama viongozi watahakikisha wanakuwa karibu na timu yao na kutimiza vyema majukumu yao ili kuhakikisha malengo yao ya kutetea mataji yote ya ndani wanayatimiza na kufika angalau hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.