Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa Paris St-Germain (PSG) ya Ufaransa, Kylian Mbappe (pichani) amerejea kwenye mazoezi ya kikosi cha kwanza na huenda hatua hiyo ikafuta rasmi mpango uliokuwa ukizungumzwa hivi karibuni wa kuihama PSG.
Taarifa fupi ya PSG ilieleza kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amerudishwa kwenye kikosi cha kwanza baada ya mazungumzo mazuri yenye kujenga na yaliyokua na mwelekeo chanya.
Mbappe aliondolewa kwenye mazoezi ya kikosi cha kwanza cha PSG na jana Jumamosi hakuwamo katika timu iliyocheza mechi ya kwanza ya Ligi 1 dhidi ya Lorient iliyomalizika kwa sare ya 0-0.
Kwa muda wote wa mechi hiyo, Mbappe alikuwa jukwaani akimshuhudia pia nyota mwenzake wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Ousmane Dembele akiiwakilisha PSG kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo kwa ada ya Pauni 43.5 milioni akitokea Barca.
Mbappe ameingia katika mgogoro na mabosi wa PSG kuhusu mkataba baada ya kugoma kusaini mkataba mpya wakati huu na awali aliachwa kwenye ziara ya PSG barani Asia iliyokuwa maalum kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi I wa 2023-24 ambao ulianza rasmi jana.
Katika siku za hivi karibuni amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na Real Madrid lakini jambo hilo halijakamilika hapo hapo Liverpool ilitangaza kuwa tayari kumsajili kwa mkopo, mpango ambao Mbappe aliukataa.
Mbappe ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya Ufaransa, pia alitakiwa na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia ambayo iliruhusiwa kufanya naye mazungumzo kabla ya kutangaza kwamba ipo tayari kuweka rekodi ya dunia kwa kumsajili kwa Pauni 259 milioni lakini Mbappe pia alikataa.
Awali mabosi PSG walimtaka Mbappe achague moja kama ni kusani mkataba na timu hiyo wakati huu au kuondoka lakini Mbappe ambaye mkataba wake wa sasa na PSG unafikia ukomo Juni mwakani alishikilia msimamo wa kutotaka kusaini mkataba mpya lakini hataki kuondoka wakati huu.
Mbappe alijiunga na PSG mwaka 2017 akitokea Monaco kwa ada ya Pauni 165.7 milioni ambayo iliweka rekodi ya usajili katika klabu hiyo, hadi sasa ameweka rekodi ya kipekee akiifungia timu hiyo jumla ya mabao 212 katika mechi 260.
Kimataifa Mbappe arejea mazoezini PSG
Mbappe arejea mazoezini PSG
Read also