Na Hassan Kingu
Mechi ya kwanza ya michuano ya Ngao ya Jamii imeisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kuzua gumzo kubwa ikiwamo Azam FC kuendelea kukubali uteja mbele ya Yanga.
Katika kipindi cha miezi 12, Yanga imekutana na Azam FC mara nne, ukiachana na ushindi wa jana, kwenye fainali ya Kombe la Azam (ASFC) imetoka kuiadhibu kwa bao 1-0 na kwenye mechi mbili za ligi, Yanga imeshinda mabao 3-2, Azam ikiambulia sare ya mabao 2-2 pekee.
Mzozo wa Fei dhidi ya Aziz Ki
Kwenye sare ya 2-2, alikuwa ni Feisal Salum wakati anaitumikia Yanga ndiye aliyeingia akitokea benchi na kwenda kuisawazishia Yanga mabao yote mawili kwa mashuti yake ya nje ya 18 lakini juzi alikuwa upande wa Azam FC na hakutosha kukata kiu ya ushindi wa timu hiyo.
Bila kificho mechi hiyo ilitawaliwa na hisia za wengi kuuona ufundi wa Fei dhidi ya waajiri wake wa zamani, Yanga lakini haikuwa hivyo na kwa mara nyingine ni Aziz Ki aliyetokea benchi na kwenda kufungua milango migumu ya Azam na kuitanguliza Yanga kabla ya Clement Mzize kuja kuhitimisha biashara.
Ikumbukwe miongoni mwa sababu zilizotajwa kuhusu kuondoka kwa Fei Yanga ni kuhitaji kuboreshewa maslahi yake ikielezwa halipwi sawasawa kulingana na shughuli yake uwanjani, ukitolewa mfano wa mchezaji kama Aziz K anayetajwa kuchota pesa nyingi na hafikii ‘shuruba’ za Fei.
Lakini jana Aziz raia wa Burkina Faso aliendelea na kazi yake ya kufunga mabao muhimu kwenye mechi muhimu na kuwakuna mashabiki wa Yanga juu ya kudhihirisha tofauti kuhusiana na mzozo wa kimaslahi uliokuwa ukizizima mno kwenye vijiwe mbalimbali vya soka nchini.
U-profesa wa Gamondi
Bado mapema mno kulinganisha utaalamu uliofanywa na Nasreddine Nabi pale Yanga na kocha wa sasa wa Wanajangwani hao, Miguel Gamondi lakini zile ‘sub’ mbili za Aziz Ki na Mzize ndio mambo tuliyokuwa tukiyaona kwa Nabi anapoamua kubadili matokeo kwenye mechi ngumu.
Ukianza na mechi ya Azam FC iliyoisha kwa sare ya 2-2, bado Nabi ana mechi lukuki, nyingine za kimataifa ambazo aliondoka na ushindi kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji kwenye kipindi cha pili.
Ubadilikaji wake kimfumo ndani ya mechi na matumizi mazuri ya benchi pana alilokuwa nalo lilitosha kumpa cheo cha uprofesa kwa wanazi wa rangi za njano na kijani.
Ya Nabi anayeendelea na ratiba zake nyingine FAR Rabat, Morocco yameshapita, na sasa tusubiri kuona Gamondi kutoka Argentina akiendeleza alichokianzisha kwenye mechi ya Azam na ile ya Kazier Chiefs aliyoshinda kwa bao 1-0 au la, ni suala la muda!
Mzize ajiongeze, kwa Mayele hapana mwenyewe
Kila mmoja anafahamu, pengo la Fiston Mayele aliyetimkia Pyramids ya Misri bado bichi mno na kupitia mechi hizi mbili dhidi ya Kaizer na Azam FC, hilo limeonekana vizuri kulingana na nafasi wanazozipata Yanga, idadi ya mabao wanayofunga na ni kina nani wamehusika.

Ni wazi Mzize ambaye bado kinda na mzawa ni wakati wake kuchangamka na kujimilikisha nafasi hiyo mapema wakati huu ambao mioyo ya mashabiki wa Yanga inasononeka juu ya nani ataziba pengo la Mayele.
Bahati mbaya, kila mmoja ametoa macho nje ya nchi, ikiaminika huko ndiko anakoweza kupatikana mbadala wa Mayele lakini kwa moto aliouwasha Mzize msimu uliopita, kwa idadi ya mechi chache alizoaminiwa kucheza, anaweza kuvaa viatu vya Mayele.
Mzize anapaswa kuelewa ufalme wa mpira haupewi tu, unatafutwa na wakati mwingine unalazimishwa kwa kuonesha makucha yako. Ni zamu yake, achangamkie fursa hasa ukizingatia kocha ni mpya, lolote linaweza kutokea.
Fei ameweka picha yake kwenye ramani
Kwa umri wa miaka sita mpaka saba aliofahamika mno Fei katika soka la Tanzania na kwa kilichotokea kwa msimu uliopita mpaka kwenye mechi ya jana, Fei ameweka alama zake ngumu katika historia ya soka nchini.
Fikiria namna alivyotoka Singida United wakati huo na kujiunga na Yanga, akiibua maswali namna alivyosajiliwa kutoka JKU ya Zanzibar kisha kwenda Yanga bila kuitumikia Singida hata mechi moja.
Na baada ya kuonesha soka safi na kuingia ndani ya mioyo ya Wanayanga, akaibua mzozo mzito siku mbili kabla ya mechi dhidi ya Azam FC, akidai amemalizana na Yanga na ni mchezaji huru, akiitaka Yanga kuidhinisha aendelee na maisha mengine ya soka.
Yanga haikuafikiana na hilo kwa kuwa bado alikuwa mchezaji wao halali kwa msimu mmoja zaidi. Rais Samia Suluhu Hassan aliiwaomba Yanga wamalize mabishano hayo na kulizima suala hilo ambapo siku chache baadae Fei akatangazwa kujiunga na Azam.
Lakini kwenye mechi yake ya kwanza ya kimashindano akiwa na uzi wa Azam, anakutana na Yanga inayowaadhibu, Fei anapigwa picha ameshika kichwa mbele ya furaha za wachezaji wa Yanga na picha hiyo inayozungumza zaidi ya tafsiri milioni moja inageuka gumzo nchi nzima na kupigilia muhuri hadithi tamu ya mchezaji huyo fundi kutoka Zanzibar.
Diarra hataki tena kuonewa na Sopu
Katika mechi nne zilizopita, Abdul Selemani ‘Sopu’ alishakutana na Yanga tangu akiwa Coastal Union na Azam na akamfunga Diarra mabao matano ikiwemo ‘hat-trick’ moja.
Mechi ya fainali ya Kombe la ASFC iliyopita, Sopu alijaribu kufurukuta na kugongesha mwamba kwenye mechi hiyo lakini hakufunga bao na kuonekana kama Diarra ilikuwa bahati yake siku hiyo ila juzi aliamua kufuta mazoea yake na Sopu na kudhihirisha ameshapata dawa ya winga huyo.
Azam FC shida nini?
Ukiachana na yote, baada ya mechi hiyo kumalizika mashabiki wengi wa soka nchini wamebaki na swali kwamba Azam FC wana shida gani kwenye kupambana na timu maarufu wenzao Afrika Mashariki?
Wapo waliofika mbali na kusema kama Yanga ingekuwa makini jana ingefunga hata mabao matano, ikionekana Azam FC ilikosa vingi vya kushabihiana na Yanga kwenye maeneo muhimu uwanjani, kwa hadhi iliyonayo Azam wengi wanategemea kuwaona wakishindana na Yanga zaidi ya walivyofanya jana.
Azam si kongwe kama Simba na Yanga lakini ina misuli ya kupambana na timu hizo, Azam ina vingi imewazidi wakongwe hao na hata kushiriki michuano ya klabu Afrika imekuwa ikipishana na wawili hao kila kukicha katika miaka ya karibuni.
Usajili wa wachezaji Azam FC unatikisa kila msimu, Matajiri hao wa Chamazi wanasifika kwa weledi kwenye nyanja nyingi dhidi ya Yanga na Simba lakini bado maswali ni lukuki wana tatizo gani haswa?
Na hii ni kwa sababu tunawaona wana kitu lakini wanakwama wapi kufika mbali? Nini kinawafanya wawe mfano wa kuigwa usiofaa kuigwa?