Paris, Ufaransa
Klabu ya PSG inadaiwa kumuondoa mshambuliaji Kylian Mbappe katika kikosi cha timu hiyo ambacho keshokutwa Jumamosi kitacheza mechi ya kwanza ya Ligi 1 msimu wa 2023-24 dhidi ya Lorient.
Uamuzi huo inaaminika umetokana na mgogoro uliopo baina ya mchezaji huyo na klabu yake ambayo inamtaka asaini mkataba mpya lakini Mbappe hataki kufanya hivyo.
Msimamo wa Mbappe ni kuendelea kuichezea PSG hadi mkataba wake wa sasa utakapomalizika Juni mwakani jambo ambalo vigogo wa klabu hiyo hawakubaliani nalo kwa hofu kwamba asiposaini mkataba wakati huu, mwakani mchezaji huyo anaweza kuondoka bila klabu hiyo kupata chochote.
Katika tukio jingine linalohusisha kuwapo kwa mgogoro baina ya Mbappe na PSG, mchezaji huyo hajafanya mazoezi na kikosi cha kwanza kilicho chini ya kocha mpya raia wa Hispania, Luis Enrique na aliachwa katika ziara ya mechi za maandalizi ya msimu nchini Japan.
Ukiacha mechi na Lorient, Mbappe pia huenda akazikosa mechi mbili zinazofuata za timu hiyo dhidi ya Toulouse na Lens kama njia mojawapo ya kumuadhibu ili akubaliane na msimamo wa klabu hiyo.
Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi ameshaweka wazi msimamo wa klabu akimtaka Mbappe asaini mkataba mpya wakati huu au aondoke.
Kwa sasa Mbappe anafanya mazoezi na wachezaji ambao wanajiandaa kuondoka PSG wakiwamo Leandro Paredes, Georginio Wijnaldum na Julian Draxler.
Tayari klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia imetangaza rasmi kumtaka mshambuliaji huyo hata hivyo mwenyewe anaonekana kuitaka zaidi Real Madrid ambayo pia inadaiwa kuhitaji huduma yake hasa baada ya kuondoka kwa Karim Benzema.
Kimataifa Mbappe azidi kutengwa PSG
Mbappe azidi kutengwa PSG
Read also