London, England
Arsenal imeanza vyema mbio za kulisaka taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2023-24 kwa kuwabwaga mabingwa watetezi wa taji hilo Man City kwa penalti 4-1 na kutwaa Ngao ya Jamii.
Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ambayo huchukuliwa kuwa ndiyo inayofungua pazia la msimu mpya wa EPL, ilipigwa Jumapili hii kwenye dimba la Wembley na kushuhudia timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 katika dakika 90 kabla ya kuelekea kwenye penalti.
Penalti ya mwisho na ya ushindi kwa Arsenal ilitiwa kimiani na Fabio Vieira wakati bao la kusawazisha la timu hiyo lilifungwa na Leandro Trossard katika dakika za nyongeza hiyo ni baada ya Man City kuandika bao la kwanza dakika ya 78 lililofungwa na Cole Palmer.
Katika penalti, mbali na Vieira wafungaji wengine wa Arsenal ni Martin Odegaard, Trossard na Bukayo Saka wakati kwa Man City waliokosa ni Kevin De Bruyne ambaye shuti lake liligonga mwamba wakati shuti la Rodri liliokolewa na kipa wa Arsenal Aaron Ramsdale.
Bao la ushindi la Vieira bila shaka litawakumbusha mashabiki wa Arsenal nyota wa zamani wa timu hiyo, Patrick Vieira ambaye mwaka 2005 pia kwenye dimba la Wembley naye alifunga bao la ushindi la penalti katika Kombe la FA.
Matokeo hayo yanakuwa mwanzo mwingine mzuri mpya kwa Arsenal katika msimu wa EPL wa 2023-24 ambao utaanza rasmi kutimua vumbi Ijumaa hii.
“Kwetu sisi ni kama tumetuma ujumbe, tumeweka alama kujijua kwamba tunaweza kuifunga Man City katika mechi kubwa pale inapobidi kufanya hivyo,” alisema kipa wa Arsenal Ramsdale.
“Sijui hali itakuwaje kwa msimu huu lakini kile kikwazo cha kisaikolojia sasa hakipo tena, tupo tayari kusonga mbele kuanzia sasa,” aliongeza Ramsdale.
Kwa Man City matokeo hayo ni majanga mengine kwenye mechi za Ngao ya Jamii baada ya kupoteza mechi hiyo mwaka 2021 mbele ya Leicester City na kupoteza kwa mara nyingine mwaka jana mbele ya Liverpool.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta pamoja na ushindi huo alitoa tahadhari akisema kwamba kwa wakati huu timu zinatakiwa kufikiria mara mbili.
“Ni lazima kujiandaa kucheza kwa dakika 100, hali hii itakuwa ikitokea kila wiki,” alisema Arteta akizungumzia dakika 13 zilizoongezwa katika mechi hiyo na timu yake kupata bao katika dakika ya 11 kwenye dakika za nyongeza.