Na mwandishi wetu
Tamasha la Simba Day limezidi kupata umaarufu baada ya klabu hiyo kumtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya klabu hiyo vilivyopatikana leo, Ijumaa mbali na wageni wengine waalikwa, kiongozi huyo mkuu wa nchi atalipamba tamasha hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa jijini, Dar es Salaam.
“Tunakushukuru na tanakukaribisha kwa furaha isiyo kifani. Kwa kipekee kabisa, tunakushukuru kwa mchango wako mkubwa kwenye michezo na maendeleo ya Taifa,” ilieleza sehemu ya taarifa ya klabu ya Simba.
Simba inafanya tamasha hilo ikiwa imetanguliwa na mahasimu wake Yanga na kufuatiwa na Singida Big, lengo mojawapo la matamasha hayo pamoja na mambo mengine ni kutangaza wachezaji wote watakaoiwakilisha timu hiyo kwa msimu mpya wa 2023-24.
Katika siku hiyo mashabiki wa Simba wataishuhudia timu yao mpya ikiumana na Power Dynamos ya Zambia, timu ambayo pia huenda ikakutana nayo tena kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya pili.
Mbali na mechi hiyo, katika tamasha hilo kama ilivyo ada kutakuwa na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali.