Na mwandishi wetu
Klabu za Simba na Yanga zimeipongeza Serikali kwa kuamua kufanya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa utakaogharimu Sh bilioni 31.
Uwanja wa Mkapa uliopo Dar es Salaam umekuwa ukitumiwa na timu hizo kama uwanja wao wa nyumbani kwa mashindano mbalimbali ya ndani na ya kimataifa.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema kuwa ni jambo la kujivunia kuona kuna mabadiliko yanakuja kwa wakati sahihi kwani kuna mashindano mengi ya kimataifa yatafanyika hapo.
“Naipongeza serikali kwa hilo kwa sababu kutakuwa na ufunguzi wa michuano ya Ligi ya Afrika kwa hiyo ubora wa uwanja ni jambo la msingi sana,” alisema.
Alisema kunapokuwa na uwanja wenye ubora hata viwango vya wachezaji vitaongezeka huku akitolea mfano Simba ilivyopanda katika viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Soka la Kimataifa (Fifa) na kuahidi kuendelea kufanya hivyo.
Kajula alisema kilichomvutia ni ukarabati wa eneo la watu mashuhuri ambalo si tu kwa ajili ya Watanzania wanaolipia fedha za ziada bali namna wanavyopanda viwango na kuwa bora wanaweza kualika watu kutoka nje ya nchi wenye uwezo mkubwa kuja kuangalia mechi na kulipa kiwango kikubwa cha fedha.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine alisema ukarabati wa uwanja ni jambo jema kwa mustakabali wa soka la nchi utasaidia timu kucheza kwa kiwango cha juu.
“Naipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuamua kufanya ukarabati wa uwanja, ni furaha kwa timu, wadau wa soka, hakika hili ni jambo la kuvutia sana na limekuja kwa mustakabali wa baadaye wa soka la nchi,” alisema Mtine
Ukarabati huo umekuja baada ya Simba kushiriki michuano ya Ligi ya Afrika (Seper League) inayotarajia kuanza hivi karibuni lakini pia Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu zilizoomba kuandaa michuano ya Afcon 2027. Nchi nyingine zinazoshirikiana na Tanzania ni Kenya na Uganda.