Na mwandishi wetu
Kiungo Mudathir Yahya amesema anajipanga vya kutosha kuhakikisha anaendelea kudumu kwenye kikosi cha Yanga msimu ujao licha ya kuwa na wakati mzuri msimu uliopita.
Mudathir amefafanua hayo akisema kwa sasa anajipanga vilivyo kwenye mazoezi ya kujiweka sawa kwani kuna wachezaji wapya wazuri wamesajiliwa, hivyo anahitaji kujiandaa zaidi ili kuonekana miongoni mwao.
“Mazoezi ya maandalizi kwa wakati huu ni muhimu sana, lazima upige sana kazi, ujipange maana kuna watu wengi wamekuja kufanya kazi, kwa hiyo usipofanya kazi utaishia kukaa nje na kusema sipendwi, sithaminiki lakini ukifanya kazi kila kitu kipo sawa,” alisema Mudathir aliyewahi kukipiga Azam FC.
Mchezaji huyo alisema kwa kuwa timu hiyo ina kocha mpya, Miguel Gamondi ni wazi kwamba kila kitu kinaanza upya hivyo ni lazima kujitahidi kuonesha kiwango sasa ili kuonesha ushawishi.
“Ukifanya masihara kipindi hiki, unaweza kukosa namba sababu wakati huu kocha anaangalia vitu vipya, haichezi historia eti kwa kuwa nimecheza fainali basi. Lazima ufanye kazi, kocha mpya akija hamjui yeyote yule, kwa hiyo cha msingi ni kuonesha kazi na kumskiliza kocha anasemaje,” alisema Mudathir.
Mudathir alisajiliwa Yanga kwenye dirisha dogo msimu uliopita kama mchezaji huru na kufanikiwa kucheza kwa kiwango cha juu akiwa miongoni mwa wachezaji tegemeo waliofanikisha Yanga kutwaa makombe matatu na kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.