Na mwandishi wetu
Mtibwa Sugar imeendelea kuimarisha kikosi chake cha msimu ujao baada ya kuwasajili Seif Karihe kutoka Dodoma Jiji FC na Abalkassim Suleiman ambaye msimu uliopita aliichezea Ruvu Shooting.
Mtibwa Sugar haijawa na mwenendo mzuri katika misimu mitatu iliyopita, kwa kulibaini hilo uongozi wa timu hiyo umepania kulitumia dirisha hili kubwa kufanya usajili wa nguvu utakaoirudisha timu hiyo kwenye ushindani.
Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru (pichani) alieleza kuwa mpaka sasa wameshakamilisha usajili wa zaidi ya wachezaji wanane, wote wakiwa ni vijana wazawa wenye vipaji vya hali ya juu.
“Msimu ujao tumedhamiria kuirudisha Mtibwa ya makombe ambayo ilikuwa na wachezaji wazawa wenye vipaji, tumekamilisha usajili wa Karihe na Abalkassim, kila mmoja akisaini mkataba wa miaka miwili lakini pia juzi tulimalizana na mshambuliaji, Matheo Anthony na beki Yassin Mustapha kutoka Singida Fountain Gate,” alisema Kifaru.
Kifaru alisema zoezi la usajili bado linaendelea na kazi hiyo wanaifanya kwa ushirikiano mkubwa na kocha wao, Habibu Kondo ambaye anashirikiana na msaidizi wake Awadhi Juma ‘Maniche’.
Kifaru alisema tayari timu yao imeanza mazoezi na Jumatatu hii walitarajia kuelekea Morogoro kupiga kambi na kucheza mechi kadhaa za kirafiki ili kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa 2023-24 wa Ligi Kuu NBC ambayo imepangwa kuanza Agosti 15, mwaka huu.
Mtibwa Sugar ilimaliza ligi msimu uliopita kwenye nafasi ya 10 ikikusanya pointi 35 na kuamua kuachana na aliyekuwa kocha wake, Salum Mayanga.