Melbourne, Australia
Tuhuma za ngono na udhalilishaji kijinsia zinazomkabili kocha wa timu ya Taifa ya Zambia, Bruce Mwape (pichani) zimesababisha kuvunjika kwa mkutano na waandishi wa habari.
Mwape ambaye anachunguzwa kwa tuhuma hizo jana Jumanne alikuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mechi yao ya Jumatano dhidi ya Hispania lakini swali kuhusu tuhuma za ngono lilisababisha mkutano huo kuvunjika hapo hapo.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya mwandishi mmoja wa habari kumtaka kocha huyo kujiuzulu kwa nia nzuri ya kutoiathiri timu na kuifanya iwe makini katika soka pekee badala ya kujadili tuhuma hizo.
“Ni mazingira yapi hasa yanayoathiri timu? Unazungumzia nini? Ningependa kufahamu kwa sababu hakuna namna yoyote ya mimi kujiuzulu bila ya kuwapo sababu,” alisema Mwape.
“Labda sababu zako zinatokana na hayo unayoyasoma kwenye vyombo vya habari au kwenye magazeti lakini ukweli wa mambo ni lazima uwekwe wazi na si uvumi,” alisema Mwape.
Swali lililofuata baada ya hilo lilikataliwa na maofisa habari wa Fifa na Zambia kabla ya mkutano huo kumalizwa na kuwaacha waandishi wa habari wakiwa hawana la kufanya.
Septemba mwaka jana Chama cha Soka Zambia (Faz) kililifikisha suala hilo Fifa kwa uchunguzi zaidi ambapo gazeti moja lilitoa taarifa baadaye likidai kwamba Mwape ni kati ya watu wanaochunguzwa kwa tuhuma hizo.
Mwape aliteuliwa kuinoa timu ya taifa ya wanawake ya Zambia mwaka 2018 na kufanikiwa kuweka rekodi ya kuiwezesha timu hiyo kufuzu kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake zinazoendelea katika nchi za New Zealand na Australia.
Katika chanzo hicho cha habari mmoja wa wachezaji aliyehojiwa ambaye hakutaja jina lake alinukuliwa akisema, “kama Mwape akitaka kulala na wewe ni lazima useme ndio.”
Zambia hata hivyo imeanza vibaya fainali za Kombe la Dunia kwa kupokea kichapo cha mabao 5-0 mbele ya Japan licha ya awali timu hiyo kuonesha kiwango kizuri na cha kuvutia katika mechi ya kirafiki ilipoilaza Ujerumani mabao 3-2.