Na mwandishi wetu
Winga mpya wa Simba, Luis Miquissone (pichani) amesema anahisi ana deni kubwa na timu hiyo kutokana na mapokezi makubwa aliyopewa na kuahidi kuipigania mpaka mwisho.
Miquissone raia wa Msumbiji ametua Simba kwa mara ya pili baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Al Ahly ya Misri hivi karibuni. Miquissone alienda Al Ahly misimu miwili iliyopita akitokea Simba.
Mchezaji huyo ambaye ametua kwenye kambi ya maandalizi ya timu hiyo iliyopo Uturuki jana Jumanne, amesema pia anaamini kwa kushirikiana pamoja, timu hiyo itafikia malengo yake msimu ujao.
“Ningependa kuwashukuru Simba na mashabiki wote kwa mapokezi mazuri niliyoyapata. Mmenifanya nihisi nina majukumu makubwa ya kuipigania klabu hii kwa kweli. Kwa kushirikiana na kufanya kazi pamoja, naamini tutafikia malengo yetu,” alisema Miquissone.
Miquissone ni miongoni mwa wachezaji pendwa wa Simba ambaye hata baada ya kuondoka kwake, pengo lake liliendelea kuonekana na sasa amerejea kwa ajili ya kuirejeshea makali timu hiyo iliyokosa makombe kwa msimu wa pili mfululizo.