Rio de Janeiro, Brazil
Beki wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Roberto Carlos (pichani) amemtaja Jay Jay Okocha kuwa ni mchezaji wa Afrika anayemvutia zaidi na ana kipaji cha wachezaji wa Brazil.
Carlos ambaye alikuwa na timu ya Brazil iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 2002, alisema anavutiwa na kipaji cha Okocha ambaye pia ni nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Nigeria au Super Eagles.
Enzi zake za soka la ushindani, Carlos amecheza dhidi ya wanasoka kadhaa nyota wa Afrika wakiwamo Samuel Eto’o na George Weah lakini anaamini kwamba Okocha alikuwa wa kipekee zaidi.
“Okocha alikuwa akicheza kama Mbrazil, alikuwa wa aina yake, baada ya kumuona akicheza katika klabu mbalimbali duniani pamoja na nchi yake, kwa maoni yangu Okocha ana kipaji cha wachezaji wa Brazil,” alisema Carlos.
“Anacheza kwa umahiri anapopiga chenga, ni ngumu kumkaba, kwa upande wangu mimi yule ndiye gwiji wa soka la Afrika,” alisema.
Okocha mbali na kuichezea kwa mafanikio timu ya Taifa ya Nigeria kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998 na 2002, pia amewahi kucheza soka Ulaya katika klabu za Frankfurt, PSG na Bolton kabla ya kustaafu soka.